KUPAMBANA HADI KUPATA USHINDI

Na Askofu Rodrick Mbwambo

Utangulizi:

Moja wapo ya maonyo yaliyotolewa na Yesu kwa wanafunzi wake wakati alipokuwa pamoja nao, ni onyo juu ya kutokukata tamaa. Yesu alisema hivyo kwa kutumia mfano wa hitaji la mwanamke maskini lililokuwa likishughulikiwa na kadhi dhalimu. Kila mara mama huyo alipolipeleka hitaji lake, kadhi huyo alionyesha kutokuwa tayari kulishughulikia. Hata hivyo pamoja na ugumu wa moyo wa kadhi huyu, bado aliendelea kumgongea yule kadhi, hadi pale alipopewa haki yake. Luka 18:2-5. Kwa kuwa kukata tamaa ni moja ya mambo yanayowazuia watoto wa Mungu kuvifikia vilele vya mapenzi ya Mungu katika maisha yao, uko umuhimu mkubwa kwa watoto wa Mungu kuelewa jinsi ya kupambana vinavyoinuka mbele zao, hadi pale ushindi unapopatikana.

Moja ya picha za watu waliopambana na hatimaye wakapata ushindi katika maisha yao, ni yule mwanamke aliyekuwa akitokwa na damu katika Israeli, kwa miaka kumi na mbili. Katika kuteseka kwake, mwanamke huyu alipambana na magumu mengi, ila kamwe hakukata tamaa. Adui alimzingira pande zote, ila alipambana hadi pale alipokutana na mapenzi ya Mungu katika maisha yake. Mambo yaliyomwezesha kupenya na kupata ushindi, yanayoweza kukusaidia hata wewe, ni pamoja na haya yafuatayo:-

KUWA NA UTAYARI WA KUPAMBANA

“Na mwanamke mwenye kutokwa na damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuwepo katikati ya mkusanyiko uliomfuata Yesu.” Marko 5:25

Kila mara wakati wa kuuendea mji wa mafanikio, viko vikwazo vitakavyoinuka ili kumzuia mwamini kukutana na yale yaliyokusudiwa na Mungu kuwepo katika barabara ya maisha yake. Mwamini atakutana na ushindi katika maisha yake, pale tu atakapoamua kupambana na vikwazo hivyo na kuvishinda. Kile ninachotaka ukione hapa ni kuwa, mafanikio yoyote yatakayomjia mtu katika maisha yake, kwa sehemu yanategemea maamuzi anayoyafanya katika maisha yake ya kila siku na aina ya maamuzi hayo. Kama maamuzi yatakuwa mabaya, maisha yake yatadidimia badala ya kwenda juu.

Hivi ndivyo ilivyotokea kwa mwanamke huyu, usugu wa tatizo lake ulitengeneza vikwazo kadha wa kadha vilivyotakiwa kuvukwa kabla ya ushindi kupatikana. Ukiiangalia hali ya mwanamke huyu muda mfupi kabla ya kumwendea Yesu, unaweza kukubaliana nami kuwa, alikuwa na kila sababu ya kutoendelea na safari yake ya kutafuta uponyaji. Hata hivyo ingawa vikwazo vilionekana kuwa vikubwa kuliko uwezo wake wa kupambana navyo, yeye aliamua kupambana navyo. Kama tunahitaji kuuona ushindi katika maisha yetu ya kiroho au yale ya kimwili, ni lazima tuanze na mhimili huu wa kufanya uamuzi mzuri.

Vikwazo ambavyo mwanamke huyu aliamua kupambana navyo, ni pamoja na hivi  vifuatavyo:-

KUPAMBANA NA VIKWAZO VYA KIDINI

“Na mwanamke kama akitokwa na damu yake siku nyingi, nayo ni katika majira ya kutengwa kwake, au kama anatokwa na damu kuzidi majira ya kutengwa kwake; siku hizo zote za kutokwa na damu ya unajisi wake, atakuwa kama alivyokuwa   katika siku za kutengwa kwake; yeye ni najisi. Kila kitanda akilaliacho katika siku zote za kutoka damu, kitakuwa kama kitanda cha kutengwa kwake; na kila kitu atakachokilalia kitakuwa najisi, kama unajisi wa kutengwa kwake. Na mtu yeyote atakayevigusa vitu vile atakuwa najisi, naye atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni.” Lawi 15:25-27

Mara nyingi katika maisha tunaweza kugundua kuwa vikwazo vinavyoongoza katika kuwazuia watu kukutana na mapenzi ya Mungu, ni vikwazo vinavyotokana na dini. Jimmy Swagart wakati fulani katika mahubiri yake alitamka kuwa, umati mkubwa wa watu watakaoingia Jehanamu, utaenda huko kutokana na vikwazo vya kidini na kitamaduni. Hivi ndivyo ilivyotukia kwa mwanamke huyu, baada ya tatizo lake kugeuka kuwa sugu, alikutana na kikwazo cha kidini kilichohitaji kuvukwa kabla ya muujiza kutokea. Mwanamke huyu  kama mwenyeji wa Mashariki ya kati na mwamini wa dini ya Kiyahudi, alijikuta katika karantini iliyotokana na andiko letu hapo juu la kutochangamana na watu kutokana na ugonjwa aliokuwa nao wa kutokwa na damu.

Mwanamke huyu angelisikia habari ya matendo makuu yaliyokuwa yakitendeka katika misafara ya Yesu ila kikwazo hiki cha kidini kilimwambia,”huruhusiwi kwenda!” Hiki ndicho kinachowatokea watu wengi katika miaka tuliyo nayo. Wanawaona wengine wakiokolewa na kupokea baraka mbalimbali za kiroho na kimwili, ila wao wanaishia kusema, “KWETU hatuokoki, hatuneni kwa lugha, hatuombei wagonjwa, na kadhalika.” Ili ukutane na mapenzi ya Mungu katika maisha yako, cha msingi ni kile kinachozungumzwa katika biblia na wala sio taratibu zinazopatikana katika tamaduni za mahali au dini. Hivi ndivyo mwanamke huyu alivyofanya, dini na utamaduni vilimwekea mipaka ila yeye akaweka juhudi za makusudi   kukivuka kikwazo hiki.

KUPAMBANA NA KUTOKUWA NA NGUVU KIFEDHA

“Amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya.” Marko 5:26

Kikwazo cha pili kilichomkabili mwanamke huyu katika kuuendea muujiza wake, kilikuwa ni kikwazo cha kutokuwa na nguvu kifedha. Ingawa huduma zilizokuwa zikitolewa na Yesu zilikuwa ni bure, bado kulikuwa na gharama ambazo wahitaji walipaswa kuzigharimia. Kwa mfano, kama mhitaji alikuwa mbali na eneo alipokuwa Yesu, ilimbidi yeye, ndugu au rafiki zake kugharimia zoezi la kumpeleka kule Yesu alipokuwa. Uhalisi wa ukweli huu, tunauona katika mojawapo ya huduma za Yesu, alizozifanya katika mji wa Kapernaumu. Baada ya habari za ujio wake kuenea kila mahali, kalamu ya Marko ilikuwa na haya ya kuandika. “Wakakusanyika watu wengi, isibaki nafasi hata mlangoni; akawa akisema nao neno lake. Wakaja watu wakimleta mtu mwenye kupooza, anachukuliwa na watu wanne.” Marko 2:1-2.

Kutokana na andiko hili, unaweza kuona kuwa, kulikuwa na gharama zilizotakiwa kulipwa ili kumfikisha mhitaji pale Masihi wa Mungu alipokuwa. Mbali na kugharimia usafiri, wakati mwingine kulikuwa kulipia gharama za chakula na malazi wakati wa kushiriki huduma zilizokuwa zikitolewa na Yesu. Marko akielezea mojawapo ya gharama hizi, aliandika yafuatayo:-  “hata zilipopita saa nyingi za mchana, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, Mahali hapa ni nyika tupu, na sasa kunakuchwa; uwaage watu hawa, ili waende zao mashambani na vijijini kando kando, wakajinunulie chakula.” Marko 6: 35-36. Kupitia mifano hii miwili, tunaweza kuona kuwa, ingawa Yesu aliwahudumia watu bure, bado kulikuwa na gharama za kibinafsi, zilizotakiwa kubewa na mhitaji. Kutokana na gharama hizi zilizotakiwa kubebwa na mhitaji, ni wazi zilitengeneza kikwazo kingine kwa mwanamke huyu aliyekuwa katika hitaji la kukutana na muujiza wake. Alitambua mahali ulipo muujiza wake, ila hali ya uchumi wake ilimwambia, huwezi kwenda huko.

Kutokuwa na nguvu za kifedha, kumewazuia watoto wengi wa Mungu kupanda ngazi za kiroho na kimwili zilizowekwa na Mungu mbele ya maisha yao. Roho Mtakatifu anaweza kuweka maono au dukuduku fulani ndani ya mtu, ila badala ya mtu huyo kuanza kuzitendea kazi dukuduku hizo, utamsikia akisema, “Sina pesa!” Waamini hawa wanashindwa kuelewa kuwa, katika mazingira ya kawaida, Mungu anapomtaka mtoto wake afanye kitu fulani kinachohitaji nguvu ya pesa, huwa haanzi kwa kumpatia mtu huyo pesa. Mungu huweka maono ndani ya mtu, na mhusika anatakiwa kuwa na utayari utakaoigeuza sifuri kuwa tarakimu iliyo na thamani. Katika hili mwamini anatakiwa akumbuke kuwa, hataulimwengu tulio nao, ulitokana na vitu visivyoonekana.

Tukirudi katika habari inayomhusu huyu mwanamke aliyekuwa na tatizo la kutokwa na damu, tunaona kuwa alikuwa anataka kufanya mradi wa kutafuta uponyaji, ila nguvu yake ya kiuchumi ilikuwa sifuri. Ingawa hali yake ya kifedha ilikuwa mbaya kiasi hicho, bado hakukiruhusu kikwazo hicho kimzuie kufanya mradi aliokusudia kuufanya. Badala yake, aliamua kufanya yale yaliyokuwa katika uwezo wake ili kufika pale muujiza wake ulipokuwa. Ni baada ya kukishinda kikwazo hiki, ndipo alipofaulu kuwa miongoni mwa umati uliokuwa ukimfuata Yesu.

Kama unahitaji kutumiwa na Mungu na kuishi kama alivyokukusudia uishi, ni lazima uhakikishe kuwa, unakishinda kikwazo hiki kinachotokana na kutokuwa na nguvu za kifedha. Kile unachotakiwa kuanza nacho katika kupambana na kikwazo hiki, ni kujitamkia kuwa, “Pamoja na kutokuwa na nguvu za kiuchumi, hakuna kitakachonizuia kuishi maisha niliyokusudiwa na Mungu, niyaishi.”

KUPAMBANA NA  MADHAIFU YA KIMWILI

“…amegharimiwa vitu vyote alivyo nayo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake, ilizidi kuwa mbaya.” Marko 5:26

Udhaifu wa kimwili ni kikwazo kingine kinachotumiwa na Shetani, kuwafanya waamini waishi maisha yanayotofautiana na vile Mungu alivyowakusudia waishi. Katika miaka tuliyo nayo, watu wengi wamemruhusu Ibilisi kutumia udhaifu wa kimwili walio nao, kuwatenganisha na mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Kuwa na udhaifu fulani katika mwili, kamwe hakutakiwi kuwa kigezo cha kumfanya mwamini asipige hatua kwenda mbele.

Katika hili nina mfano ulio wazi wa mtu, aliyemkatalia shetani kuutumia udhaifu wa mwili wake kumtenganisha na kusudi la Mungu katika maisha yake. Mtu huyu alizaliwa bila mikono na miguu, ila bado anaweza kucheza mpira kwa kutumia kichwa, anaweza kuogelea, pamoja na amefanikiwa kupata ujuzi unaompatia riziki yake ya kila siku. Hivi ndivyo ilivyotukia kwa mwanamke huyu aliyekuwa katika harakati za kukutana na muujiza wake, ingawa ugonjwa ulimfanya kuwa nusu mfu, bado alifanikiwa kupenyeza katikati ya umati mkubwa wa watu na kugusa vazi la Yesu.

Ni kweli udhaifu wa mwili, unaweza kumzuia mtu kuwa na kasi ya   mtu asiye na tatizo katika mwili wake, ila hauwezi kumzuia kwenda kwa kasi iliyoandaliwa na Mungu kwa ajili yake. Katika hili, ninaamini kuwa, ‘Mungu ameandaa vilele vya   baraka kwa kila mtu na umbali wa kuvifikia vilele hivyo, unategemea vile uwezo wa mtu ulivyo.’ Kama unataka bendera ya maisha yako ya kiroho na kimwili ipepee, fanya kile kilichofanywa na mwanamke huyu. Yeye aliuangalia udhaifu aliokuwa nao kimwili na kusema, “Muda wote Yesu aishipo, bado lingaliko tumaini.”

KUPAMBANA KIKWAZO CHA UPWEKE

“Na mwanamke kama akitokwa na damu yake siku nyingi, nayo ni katika majira ya kutengwa kwake, au kama anatokwa na damu kuzidi majira ya kutengwa kwake; siku hizo zote za kutokwa na damu ya unajisi wake, atakuwa kama alivyokuwa   katika siku za kutengwa kwake; yeye ni najisi. Kila kitanda akilaliacho katika siku zote za kutoka damu, kitakuwa kama kitanda cha kutengwa kwake; na kila kitu atakachokilalia kitakuwa najisi, kama unajisi wa kutengwa kwake. Na mtu yeyote atakayevigusa vitu vile atakuwa najisi, naye atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni.” Lawi 15:25-27

Mara zote tatizo la mtu linapokuwa sugu, huwa ni rahisi mno kwake kukumbwa na roho ya upweke. Kwa mfano, kulingana na sheria ya Musa, mtu aliyekuwa na ugonjwa wa kutokwa na damu muda mrefu, huyo hakuruhusiwa kuchangamana na watu wengine waliokuwa wazima. Kwa maneno mengine, ugonjwa uliomkabili mwanamke huyu, ulimweka katika kifungo kibaya mno cha upweke. Mfano mwingine unaoonyesha vile matatizo sugu yanavyotengeneza upweke kwa mtu, tunaupata katika andiko lifuatalo; “Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, alimwambia, Wataka kuwa mzima? Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani..” Yohana 5:6-7.

Kutokana na upweke huu unaozaliwa pale tatizo la mtu linapokuwa sugu, waamini wengi wameshindwa kumzalia Bwana matunda. Kama hili halitoshi, waamini wengi wachanga wamerudi nyuma kiroho, kutokana na roho hii ya upweke. Hata waamini wengi wachanga wanashindwa kuendelea na maisha ya wokovu, kutokana na upweke. Wako pia kinamama waliofikia hatua ya kujinyonga baada ya kufiwa na waume zao pale waliposhindwa kupambana na roho hii ya upweke.  Roho ya upweke iko kwa baadhi ya vijana waliopoteza wachumba wao, kwa ushirika uliopoteza mchungaji wake, mume aliyepoteza mke wake na kwa wanafunzi walio mbali na wazazi wao. Pamoja na kikwazo hiki cha upweke, ushindi uko katika kupambana nacho hadi kukishinda.

Hivi ndivyo alivyofanya mwanamke huyu, tunayejifunza kupitia maisha yake katika injili ya Marko. Ukiangalia mazingira yatatizo lake kama yanavyoonekana katika andiko letu hapo juu, unaweza kuona kuwa, ni mwanamke aliyekuwa katika upweke usiopimika kwa mizani wala kwa shubiri. Kama tulivyoona katika vipengele vilivyopita, utamaduni na dini yake vilikuwa havimruhusu kuchangamana na watu, pili, alimwendea Yesu Kristo bila kuwa na mtu wa kumsindikiza. Ingawa alikosa mtu wa kumshika mkono wala kumtia moyo, yeye hakukubali hali hii imkatishe tamaa. Mwanamke huyu aliitumia imani yake kama mkongojo na kusema, “kwa ‘mkongojo’ huu, nitakutana na mapenzi ya Mungu katika maisha yangu.”

Ndugu yangu, kama unakabiliwa na tatizo sugu, na tatizo hilo limekufanya uwe mpweke, napenda kukutia moyo kuwa, kwa msaada wa Mungu, unaweza kuushinda upweke unaokukabili. Jambo la kwanza ushindi utakujia kwa kutambua kuwa, upweke ni moja ya silaha zinazotumiwa na Ibilisi kuwazuia watoto wa Mungu kula mema ya nchi. Ukiujua ukweli huu, utapambana na kikwazo hiki, badala ya kukaa mkao wa kulegea kana kwamba huna la kufanya. Ukweli wa tatu unaotakiwa kuutambua ni kuwa, mara zote upweke kwa watoto wa Mungu sio kitu kilicho halisi. Kamwe haitatokea mtu aliyeokoka na kuishi sawasawa na mapenzi ya Mungu, kuwa katika hali ya upweke. Hili nalisema kutokana na sababu kubwa mbili. Sababu ya kwanza, Mungu katika neno lake, tayari ameshatamka kuwa, “Yuko pamoja nasi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” Mathayo 28:20. Pili, sambamba na Mungu kuwa pamoja na mwamini nyakati zote, mwamini ni sehemu ya familia ya Mungu.

Familia hii iko katika makundi makubwa mawili. Kwanza, ni ile familia ya waamini wanaoishi katika eneo moja la kijiografia naye, inayojulikana kama kanisa la Mungu la mahali (local church). Kundi la pili, ni la waamini wanaoishi katika maeneo mengine ya kijiografia yaliyo mbali na mwamini, wanaojulikana kama kanisa la Kristo la kiulimwengu (universal church). Kwa vile waamini wote ni viungo vya mwili wa Kristo, ni uongo pale Shetani anapompandikizia mwamini roho ya upweke na kumtaka kuuamini uongo huo. Katika hali zote mwamini anatakiwa atambue kuwa, wako waamini wanaomjua na wasiomjua wanaomwombea kwa mzigo. Kupitia ufahamu na ukweli huu, ukatae uongo huu wa Shetani na utamke kwa ujasiri kuwa, kama mwanamke huyu ambaye hakuwa mwamini aliweza kuushinda upweke na kupokea muujiza wake, mimi kama mtoto wa Mungu, nitashinda pia kile kinachoonekana kuwa upweke katika maisha yangu.

KUPAMBANA NA VIZUIZI VINAVYOLETWA NA WATU

“Na mwanamke mwenye kutokwa na damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuwepo katikati ya mkusanyiko uliomfuata Yesu.” Marko 5:25 Kikwazo kingine kilichomkabili mwanamke huyu, ni umati mkubwa uliokuwa umemzunguka Yesu, katika safari yake ya kwenda kumponya binti Yairo. Kupitia miujiza miwili iliyofanywa na Yesu ya kuwalisha watu, yawezekana kwa uchache umati uliokuwa ukimfuata Yesu, ulikuwa haupungui watu 10,000. Kutokana na umati huu, ilikuwa ni vigumu mno kwa wagonjwa waliozidiwa kumfikia Yesu na kukutana naye uso kwa uso. Wakati mwingine ilimbidi mhitaji au ndugu zake watumie nguvu za ziada, ili kuifikia mikono ya Yesu. Mfano mzuri katika hili, ni ule unaomhusu mwenye kupooza, aliyepelekwa kwa Yesu na watu wanne katika injili ya Marko. Kutokana na umati uliokuwa unamsonga Yesu, iliwabidi wale waliomchukua wavunje dari ili wapate nafasi ya kumtelemsha mgonjwa wao pale Bwana wa uponyaji alipokuwa. Marko 2:4.

Mfano wa pili, ni huu wa huyu mwanamke aliyekuwa akitokwa na damu kwa miaka 12 mfululuzo. Kutokana na  udhaifu katika mwili wake, ni wazi ilikuwa vigumu mno kwake kupenya katikati ya umati wa watu, hadi kufika pale Yesu alipokuwa. Kitu cha kutia moyo ni kuwa, pamoja na ugumu huu, bado aliweza kupenya na kushika vazi la Yesu. Tunachojifunza katika mifano hii miwili ni kuwa, watu wanaweza kumsaidia mwamini kupata ushindi, na wakati mwingine  wanaweza kuwa kikwazo cha kumzuia mtu kukutana muujiza wake. Kwa mfano, mwenye kupooza katika mlango wa kondoo katika injili ya Yohana, alishindwa kufunguliwa mapema, kutokana na kukosa mtu wa kumwingiza birikani. Yohana 5:2-7. Tukija kwaBartimayo yule kipofu, mambo yalikuwa kinyume, yeye watu ndio waliojaribu kuuzuia muujiza wake!

Kwa yeyote yule anayetaka kupata upenyo na kumliza yule aliyekuwa akimliliza, anatakiwa afanye uamuzi wa kupambana na Shetani mpaka pale ushindi atakapopata majibu ya maswali yake. Hivi ndivyo huyu mwanamke alivyofanya, umati ulikuwa kikwazo kikubwa kwake, ila aliweka bidii ili kukishinda kikwazo hiki kwa lengo la kuutwaa muujiza wake.

KUWEKA BIDII YOTE KATIKA KUPAMBANA

“Na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu WENGI…” Marko 5:26

Jambo lingine lililochangia kumletea mwanamke huyu ushindi, ni ile bidii aliyokuwa nayo katika kupambana na tatizo alilokuwa nalo. Tatizo lilipompata, alihakikisha kuwa anawaendea madaktari wote aliokuwa anawafahamu, kwa lengo la kutafuta uponyaji. Tunapozama ndani katika kipengele hiki, ninataka utambue kuwa, katika ulimwengu tulio nao, kamwe hakuna mtu aliyeandikiwa na Mungu kuishi maisha mabaya. Mungu kama Muumbaji mwenye upendo,  ametengeneza barabara nzuri za maisha kwa kila mtu, ila mtu mwenyewe, ndiye anayeweza kuamua kutembea ndani au nje ya barabara hiyo.

Kwa mfano, mtu anapoukataa wokovu, hamkatai tu Kristo, bali, anayakataa pia mapenzi ya Mungu katika maisha yake. Hali kadhalika, mtu aliyemwamini Kristo na hatimaye akalegea katika kupambana na vikwazo vinavoinuka katika maisha yake, huyo naye atakuwa mbali na mpango wa Mungu wa neema, ulikusudiwa kuwa katika maisha yake. Ulegevu tunaouongelea hapa, ni ule wa kutotumia NGUVU zote, MOYO wote na ROHO yote katika kumwishia na kumtumikia Mungu. Roho hii ya kufanya mambo nusu nusu, ndiyo iliyomfanya mfalme wa Israeli, ashindwe kuangamiza majeshi ya mfalme wa Shamu. Nabii alimwambia kupiga mshale chini, yeye akapiga mara tatu na kuacha. Alipoacha Elisha alimwambia maneno yafuatayo; “Ingelikupasa kupiga mara tano au mara sita; ndipo ungaliipiga Shamu hata kuiangamiza; bali sasa utaipiga Shamu mara tatu tu.” 2 Wafalme 13:19.

Tukiingia ndani ya kanisa la siku hizi za mwisho, tunaweza pia kuona kuwa roho hii ya kufanya mambo kwa kutumia nguvu kidogo, ndiyo inayoifanya idadi ya wafuasi wa imani ya Kikristo, kukaribia ile ya Waislamu wakati ambapo Uislamu, ulianza karine tano baada ya Ukristo kuanza. Kiongozi wa kanisa la mahali, anaweza kuhamasisha waamini kwenda kushuhudia, ila  baadaye, utawakuta waamini hao wakirudi mikono mitupu bila mavuno. Kama atatokea wa kuuliza kulikoni, mara zote jibu linakuwa rahisi, “hatukupata mtu leo!” Hata hivyo ukiliangalia zoezi zima la huo ushuhudiaji, utagundua kuwa, waamini hao hawakutumia nguvu zao zote katika kulifanya zoezi hili. Udhaifu huu, uko pia katika maeneo ya ufuatiliaji, utoaji, uimbaji na kadhalika; ndio watu wanafanya, ila sio kwa kutumia nguvu zao zote.

Kwa mwanamke huyu tunayemzungumzia katika habari yetu, hakuridhishwa na madaktari wawili au watatu, wakati wa kutafuta muujiza wake. Yeye alitumia nguvu yote ya fedha aliyokuwa nayo, kutafuta tiba ya tatizo lake. Hata tunapoangalia Biblia, tunaona kuwa, watu waliotumiwa kwa namna ya kipekee na Mungu, ni wale walioweka bidii ya kutosha katika shughuli za kiroho na zile za kimwili. Mfano mzuri wa watu hawa, ni wanafunzi wa Yesu. Wao hawakumfuata Yesu nusu nusu, bali walimfuata kwa mioyo yao yote na kujitoa kwao ndiko kulikomfanya Petro atamke kuwa, “Sisi tumeacha vyote tukakufuata.” Marko 10:28.

Kama waamini wa siku za mwisho wanataka kuuona mkono wa Mungu, katika maisha yao ya kiroho na kimwili, ni lazima watumie bidii yao yote kutafuta mambo ya rohoni nay ale ya kimwili. Kwa maneno mengine, kama nguvu za wanadamu zingelikuwa sawa na mipira ya manati, wanatakiwa wajivute mpaka ifikie kikomo cha kuvutika kwake.

KUTOKUBALI KUKATA TAMAA

“Na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya; aliposikia habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyumba, akaligusa vazi lake.” Marko 5:26

Kitu kingine kilichomsaidia mwanamke huyu kusonga mbele hadi kuufikia muujiza wake, ni ile roho aliyokuwa nayo ya kutokukata tamaa. Andiko letu hapo juu, linaonyesha vile kibinadamu, mwanamke huyu alivyokuwa na kila sababu ya kukata tamaa. Katika kupambana na tatizo alilokuwa nalo, alipitia waganga wengi, pochi yake ilikuwa tupu, ila kulingana na andiko letu hapo juu, bado aliendelea kutafuta waganga. Ni katika kutafuta huku, ndipo alipokutana na Mganga wa waganga, aliyeweza kumwondolea mzigo uliokuwa ukimlemea. Kama angelikata tamaa, angelibakia nyumbani na hapo angelikufa kile kifo Waswahili wanachokiita, ‘kifo cha kiofsa.’

Kuifungulia roho ya kukata tamaa, kumechangia mno kuzorotesha maendeleo ya kiroho na ya kimwili ya watoto wa Mungu. Mtu anaweza kumpokea Yesu leo na kesho tu anataka kuwa mhubiri kama Billy Graham au Reinhard Bonke. Hali kadhalika, kama ni mafanikio ya kimwili, nayo wanataka yaje mithili ya kumulika kwa radi. Yale wanayoyatarajia yasipokuja kwa wakati wanaoutaka, wanaamua ‘kuozea’ katika mkeka wa kukata tamaa. Wakati umefika kwa waamini kujifunza kutokata tamaa kutoka kwa watu maarufu kama vile Thomas Edson. Mskotishi huyu, alijaribu kutengeneza balbu za umeme zaidi ya mara 2,000 bila mafanikio na hapo, wakatokea watu wengi walimtembelea kwa lengo la kumkatisha tamaa. Hata hivyo, kama ilivyokuwa kwa Ayubu mbele za wataabishaji wake, mtu huyu alikataa kabisa kuifungulia mlango roho ya kukata tamaa   na leo bulbu za umeme zimeenea dunia nzima.

Kama watoto wa Mungu wa kanisa la siku za mwisho wanataka kuishi maisha ya ushindi, wanatakiwa kukataa kwa gharama yoyote ile, roho hii ya kukata tamaa.

KUUONA USHINDI KABLA HAUJATOKEA

“Maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona.” Marko 5:28

Andiko hili linatuonyesha kiwango cha imani kilichokuwa ndani ya mwanamke huyu. Kama vile Yona alivyomtukuza Mungu akiwa ndani ya tumbo la samaki, ndivyo alivyofanya. Imani ya kupokea aliyokuwa nayo, ilimpelekea kuamini kuwa, pale tu atakapolishika vazi la Yesu, atapona msiba aliokuwa nao. Tunachokiona kwa mwanamke huyu ni kuwa, aliamini shuhuda zote alizozisikia kuhusiana na matendo makuu yaliyofanywa na Yesu na akazigeuza shuhuda hizo kuwa pumzi ya mapafu yake. Kwa maneno mengine, tunaweza kusema kuwa, ujazo wa shuhuda za matendo makuu ya Yesu, ulijaa ndani yake kiasi cha kutobakia nafasi ya mashaka ndani ya roho na ufahamu wake. Imani hii ya kupokea, ndiyo iliyomfanya auone ushindi dhidi ya tatizo alilokuwa nalo, hata kabla ya kukutana na Yesu.

Kama wewe ni mmoja wa wale wanaotaka kula mema ya nchi, itakulazimu, uruhusu aina hii ya imani kuumbika ndani yako. Mambo yote yaliyoletwa na Mungu duniani kupitia kwa Yesu Kristo, yanapatikana kwa imani. Kama vile milango mitano ya ufahamu inavyomwezesha mtu, kuwa na uhakika wa mambo yaliyopo katika ulimwengu wa kimwili, kwa imani mwamini anakuwa na uhakika wa kile kinachofanyika katika ulimwengu wa kiroho kuhusiana na maisha yake. Kupitia jicho la imani, Yusufu aliuona ukombozi wa wana wa Israeli kutoka Misri na kuwaagiza akisema, “Bila shaka Mungu atawajia ninyi, nanyi mtaipandisha huko mifupa yangu.” Mwanzo 50:25. AMENI!