USHIRIKA WA ARUSI YA KANA

Na Askofu Rodrick Mbwambo

Utangulizi:

Kana katika karine ya kwanza, kilikuwa ni kijiji miongoni mwa vijiji katika wilaya ya Galilaya. Ni katika kijiji hiki ndipo tunapokutana na muujiza wa kwanza alioufanya Yesu, katika huduma yake, wa kugeuza maji kuwa divai. Hali kadhalika  katika kijiji hiki ndipo Yesu alipokutana na diwani aliyemjia ili aende Kapenaum, kumponya mtoto wake. Badala ya Yesu kwenda naye, alimwambia kuwa aende nyumbani na binti yake atakuwa mzima na ikawa hivyo.

Katika somo la leo, ninataka tuangalie mambo kadha wa kadha, yanayohusiana na ule mkusanyiko uliozaa muujiza wa kwanza katika huduma ya Yesu. Biblia inapozungumza juu ya mkusanyiko huu, inasema kuwa, ulikuwa ni mkusanyiko ulioandaliwa mahususi kuwaunganisha watu wawili mke na mume, kuwa mwili mmoja. Kutokana na uhusiano uliopo kati ya kanisa na arusi, mkusanyiko huu kwa sehemu, tunaweza pia kuupa sura ya kanisa la mahali la Kristo. Tunapoliangalia kusanyiko hili, tunaweza kuona kuwa, mwanzoni lilikabiliwa na tatizo lililotishia kuvuruga kusudi la mkusanyiko, ila baadaye, ushindi uliweza kupatikana. Ili kanisa la siku hizi za mwisho liweze kufanikisha lengo kuu la kuchaguliwa kwake, ni lazima liishi katika mazingira yanayofanana na yale yaliyokuwepo katika mkusanyiko wa arusi ya Kana. Mazingira tunayoyazungumzia hapa, ni pamoja na haya yafuatayo:-

MAZINGIRA YA  MIALIKO

“Na siku ya tatu palikuwa na arusi huko Kana, mji wa Galilaya, naye mama yake Yesu alikuwapo. Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake.” Yohana 2:1-2

Kupitia andiko hili tunaona kuwa kitu cha kwanza kilichofanikisha mkusanyiko wa arusi hii iliyofanyika katika kijiji cha Kana ya Galilaya, ni ile mialiko iliyopelekwa kila mahali, kuwaita watu kushiriki katika arusi hii. Leo hii andiko hili la arusi ya Kana ya Galilaya, limepata nafasi ya kuwa sehemu ya neno la Mungu, kutokana na mialiko na kupokelewa kwa mialiko hiyo.   Mwaliko ulimleta Yesu na mama yake katika mkusanyiko ule, na uhitaji ulipotokea, waalikwa hawa, waliweza kulimaliza tatizo hilo.

Kutokana na mazingira ya mialiko kufanikisha mkusanyiko huu katika Kana ya Galiya, ni wazi arusi kati ya Yesu na kanisa itafanikiwa tu, pale wale waliokwisha kuingia katika arusi hii watakapowaalika wengine kujiunga na arusi hii. Mtu asiyeweka bidii kuwakutanisha wengine na Yesu, huyo hatakuwa na sifa ya kuitwa bibi arusi wa Mwanakondoo wa Mungu. Filipo alipokutana na Yesu, alimwalika Nathanaeli, yule mama Msamaria naye alipokutana na Yesu, aliwapelekea wengine mwaliko ili waje wamwone Yesu. Yohana 1:44-45, Yohana 4:28-29. Ushirika (kanisa) utakaofanikiwa katika kuupendeza moyo wa Mungu, ni ule unaojishughulisha kwa kila hali, kuwaleta wengine kwa Yesu.

MAZINGIRA YA SHEREHE

“Walipokuwa katika kusherehekea, divai ikawaishia, na mama yake Yesu akamweleza Yesu juu ya tatizo hilo.” Yohana 2:3 (LBE)

Biblia inasema kuwa, wakati sherehe ilipokuwa imenoga, hapo divai ikawatindikia. Kila mara mkusanyiko unaoweza kufanya mambo ya kushangaza na kuupendeza moyo wa Mungu, ni ule unaotawaliwa na mazingira ya sherehe. Lazima uwe mkusanyiko ambao kila mmoja anafurahia kile anachokifanya, hali kadhalika, kufurahia kile anachofanyiwa na wengine. Kanisa la siku za mwisho kwa kiwango kikubwa limeshindwa katika kuutumikia utume mkuu, kutokana na mazingira haya. Leo hii katika sharika nyingi, waamini wengi wanaishi katika sheria na kushinikizwa kutumika, badala ya kufunikwa na mazingira ya sherehe.

Ili kanisa la siku za mwisho liweze kumpendeza Mungu, kila mwamini anatakiwa kutawaliwa na mazingira ya sherehe katika kuishi kwake. Kama ni kuhudhuria ibada, ahudhurie kwa vile anafurahia kufanya hivyo na kama ni kujitolea nguvu, vipawa na mali zake, afanye hivyo kwa vile moyo wake unafurahia kufanya hivyo.

MAZINGIRA YA KUTINDIKIWA

“Walipokuwa katika kusherehekea, divai ikawaishia, na mama yake Yesu akamweleza Yesu juu ya tatizo hilo.” Yohana 2:3 (LBE)

Nirudie tena kuwa, muujiza wa kwanza kufanywa na Yesu rasmi katika huduma yake, ni huu alioufanya katika mkusanyiko wa arusi ya Kana ya Galilaya. Hata hivyo ukiuangalia muujiza huu, utaona kuwa, kamwe usingeliweza kufanyika kama kusingelikuwa na mazingira ya kupungukiwa. Kwa maneno mengine, tunaweza kusema kuwa, ushirika unaojihisi kutosheka, kamwe hauwezi kufanikiwa katika kuyafanya mapenzi ya Mungu.

Kanisa la siku hizi za mwisho ni lazima liwe kusanyiko lisilojitosheleza hivyo kumhitaji Mungu ili alitosheleze. Mahali popote pale ambapo watu wanadhania kuwa wanajitosheleza, Mungu hana nafasi katika kusanyiko hilo. Kwa maneno mengine, mtu yeyote anayehitaji kuishi sawasawa na mapenzi ya Mungu, anatakiwa awe na  kilio cha kupokea zaidi kutoka kwa Mungu. Kilio hiki kinapokuwepo, mwamini atakuwa mtendaji wa neno katika hali zote.

MAZINGIRA YA KUTATUA MATATIZO

“Walipokuwa katika kusherehekea, divai ikawaishia, na mama yake Yesu akamweleza Yesu juu ya tatizo hilo.” Yohana 2:3 (LBE)

“Yesu akawaambia watumishi, jazeni mabalasi maji, nao wakayajaliza hadi juu. Kisha akawaambia, sasa choteni kiasi mumpelekee mkuu wa meza.” Yohana 2:7 (NIV)

Mazingira mengine tunayokutana nayo katika mkusanyiko huu wa arusi ya Kana, yanatokana na kile kilichofanyika baada ya tatizo kutokea. Baada ya tatizo kutokea, kusanyiko hili halikukaa na kuanza kumlilia Mungu ili aliletee mtu atakayelitatua tatizo hilo. Badala yake, tunaona kuwa, mara tu baada ya tatizo hilo kutokea, wale walikuwepo katika mkusanyiko huo, walianza kupambana na tatizo hilo. Kwanza, Mariamu mama yake Yesu, alimwendea Yesu na kumfahamisha juu ya tatizo hilo na baadaye, Yesu naye, aliwaeleza watumishi la kufanya.

Kanisa la Mungu katika siku hizi za mwisho nalo, linatakiwa lifanane na mkusanyiko huu wa arusi ya Kana, kwa kuelewa cha kufanya, pale matatizo yanapotokea. Kama tatizo ni jinsi ya kupata jengo la kuabudia, kamwe waamini wasikae mkao wa kungojea mfadhili wa kufanya hivyo. Katika kila hitaji litakaloonekana katika mkusanyiko wa watu wa Mungu, wanatakiwa wawepo waamini watakaoshugulisha akili na viungo vyao na kulitolea hitaji hilo majibu. Kamwe mkusanyiko wa watu wa Mungu, hautakiwi kuwa mahali, pa kudondosha machozi yasiyo na majibu.

MAZINGIRA YA UTII

“Mamaye akawaambia watumishi, lolote atakalowaambia, fanyeni.”   Yohana 2:5

“Yesu akawaambia watumishi, jazeni mabalasi maji, nao wakayajaliza hadi juu. Kisha akawaambia, sasa choteni kiasi mumpelekee mkuu wa meza. ” Yohana 2:7-8 (NIV)

Jambo lingine lililoleta utoshelevu katika mkusanyiko wa arusi ya Kana, ni mazingira ya utii. Tunapoyaangalia maandiko yetu hapo juu tunaweza kuona kuwa, kila aliyeagizwa kufanya kitu wakati tatizo lilipotokea, aliweza kutii na kufanya sawasawa na vile alivyoagizwa. Kwa mfano, mkuu wa meza alikuwa anahitaji divai, ila Yesu akawaagiza wahudumu katika sherehe ile kumpelekea maji! Agizo hapa halikuendana kabisa na hitaji la mkuu wa meza, ila watumishi walitii na kufanya hivyo. Kile tunachojifunza hapa ni kuwa, kama kusingelikuwa na mazingira ya kutii katika mkusanyiko huu, ni wazi muujiza tunaousimulia, usingelitokea.

Kanisa la Mungu nalo, linatakiwa kuwa na waamini walio tayari kutii katika mazingira yoyote yale. Mazingira ya kutii yalimbadilisha Abramu na kuwa Ibrahimu, yaliifanya sadaka ya Habili ipokelewe, yalimwezesha Petro kutoa shekeli tumboni mwa samaki na yalimfungua kipofu pale alipoenda kujiosha katika ziwa la Siloam.

Kinyume cha kutii ni ile hali ya kutokutii inayotawala leo katika kanisa la siku hizi za mwisho. Kazi ya Mungu katika miaka yetu, kwa kiwango kikubwa, imevurugwa na roho hii ya KUTOKUTII ndani ya kanisa la Kristo. KUTOKUTII kumewafanya watumishi kuishi kama ombaomba kutokana na waamini kutoleta zaka kamili na matoleo mengine katika nyumba ya Mungu. Kama hili halitoshi, KUTOKUTII ndiko kunakoufanya ulimwengu kuwa na makundi ya watu wasiyofikiwa na Injili, licha ya miaka zaidi ya 2000 ya Injili duniani. Kama kanisa linahitaji kuupendeza moyo wa Mungu, linatakiwa kuwa na waamini wanaokubaliana na kile kilichozungumzwa na Mariamu pale aliposema, “lolote atakalowaambieni, fanyeni.”

MAZINGIRA YA USHUHUDA

“Naye mkuu wa meza alipoyaonja yale maji yaliyopata kuwa divai (wala asijue yalikotoka ila watumishi walijua, wale walioyateka yale maji), yule mkuu wa meza alimwita bwana arusi, akamwambia, Kila mtu kwanza   huandaa divai iliyo njema; hata wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka divai iliyo njema hata sasa.” Yohana 2:9-10

Mazingira mengine yanayotakiwa kutawala kanisa la siku za mwisho, ni mazingira ya USHUHUDA. Andiko letu hapo juu linatueleza kuwa, wale walioionja ile divai, walimwendea bwana arusi na kumpongeza kwa kuanza na kuimaliza sherehe kwa divai njema! Mazingira haya ni tofauti kabisa na kile kinachotendeka ndani ya sharika nyingi za kanisa la siku hizi za mwisho. Katika sharika hizi, kiongozi anaweza kutumia zaidi ya dakika kumi, kuwahamasisha waamini juu ya umuhimu wa kushuhudia yale waliyofanyiwa na Mungu katika maisha yao ya kila siku. Wakati mwingine, inabidi wimbo maalum uimbwe ili kuwahamasisha waamini kushuhudia. Katika mkusanyiko wa arusi ya Kana ya Galilaya, mambo yalikuwa tofauti. Wao walipoionja divai, waliwatangazia wengine juu ya kazi nzuri, iliyofanywa na bwana arusi!

Kanisa la Kristo linatakiwa kuonyesha shukrani na tabasamu, pale linapoziona kazi za Mungu zikitendeka katikati yake.   Utayari huu katika kushuhudia, utamwonyesha Mungu kuwa Yeye yuko mbele katika maisha yetu na ya kuwa, bila yeye hatuwezi kufanya neno lolote. Kanisa linapopungukiwa na wepesi katika kushuhudia, linauonyesha ulimwengu kuwa, halimhitaji Mungu kwa vile linajitosheleza lenyewe.

MAZINGIRA YA NJEMA INAYODUMU

“Akamwambia, Kila mtu kwanza   huandaa divai iliyo njema; hata wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka divai iliyo njema hata sasa.” Yohana 2:9-10

Andiko letu hapa juu linazungumzia juu hali halisi iliyokuwa ikiikabili mikusanyiko ya arusi, zilizokuwa zikifanyika katika Mashariki ya kati. Katika mikusanyiko hiyo, kulikuwa na divai njema isiyodumu. Kutokana na gharama, bwana arusi angeliweza kutanguliza divai iliyo njema na baada ya watu kunywa kwa muda mrefu, huleta divai iliyo dhaifu. Katika mkusanyiko wa arusi ya Kana, mambo yalikuwa tofauti; sherehe ilianza na divai njema na kisha, ikamalizika na divai njema.

Hivi ndivyo mambo yanavyotakiwa kuwa katika mikusanyiko ya watu wa Mungu. Kwa kuwa Yesu Kristo, ni yeye yule jana leo na hata milele, mema katika mikusanyiko ya watu wa Mungu, hayatakiwi kuwa mambo ya msimu. Kama mwamini amefanikiwa kufikia kasi fulani kimaombi, utoaji au kuwaleta wengine kwa Bwana, anatakiwa aichunge kasi hiyo isije ikapungua. Hali kadhalika, kama karama na upako vimeanza kujidhihirisha ndani ya mwamini, hali hiyo inatakiwa kuchungwa mithili ya moto katika madhabahu ya hekalu la Bwana. Lawi 6:13

Mkusanyiko wa kweli wa watu wa Mungu, ni lazima uwe na bidii isiyopungua katika kumwishia Mungu.

Naamini kuwa somo hili limeleta changamoto kubwa sana kwako na kwa kanisa lako la mahali. Nikukumbushe tu vile Biblia inavyosema kuwa, mtu anayepata ufahamu bila kuutendea kazi ufahamu huo, huyo atawekwa katika kundi la watu wasio na hekima. Kwa kuwa wewe ni mwenye hekima, basi ENENDA UKAWE MTENDAJI WA NENO! AME