Somo la 2: MAISHA NDANI YA EDENI NA ANGUKO (Imerudiwa)
Na Askofu Rodrick Mbwambo
Baada Mungu kuwaumba wanadamu, aliwatengenezea bustani na akawaweka ndani ya bustani hiyo. Inawezekana kuwepo kwa bustani hiyo katika nchi ya Edeni, ndiko kulikoisababishia kuitwa bustani ya Edeni. Basi BWANA Mungu alikuwa ameotesha bustani upande wa mashariki, katika Edeni, huko akamweka huyo mtu aliyemwumba (Mwanzo 2:8).
WAJIBU NDANI YA BUSTANI YA EDENI
Kitu cha kwanza ambacho Mungu aliwapa wanadamu baada ya kuwaweka katika bustani yake, ni wajibu. Wajibu huu ulikuwa na mambo makubwa mawili, kuilima na kuitunza bustani hiyo. BWANA Mungu akamchukua huyo mtu akamweka kwenye bustani ya Edeni ailime na kuitunza (Mwanzo 2:15. Kwa kuwa wakati huo kulikuwa hakuna magugu wala kitu chochote kinachoweza kuharibu mazao, ni wazi wajibu huu ulikuwa unamaanisha, kuiendeleza bustani hii hadi ifunike nchi yote ya Edeni.
Wajibu huu, unatuonyesha jinsi Mungu anavyofanya kazi, huteua kitu kidogo ili kizae kitu au jambo lililo na ukubwa wa kushangaza. Alipandikiza bustani ndogo kwa ajili ya mwanadamu na kumtaka aiendeleze katika nchi yote ya Edeni. Kutokana na ukweli huu, kama unafanya jambo lo lote linaloufurahisha moyo wa Mungu, jambo hilo litapanuka na kuwa kubwa, hata kama kwa sasa linaonekana kuwa dogo.
Jambo lingine, tunalojifunza katika maandiko haya, ni umuhimu wa kuwajibika katika ufalme wa Mungu. Kuwajibika, ni kwa muhimu sana katika uhusiano kati ya Mungu na mwanadamu. Baadhi ya watu wanadhania kuwa kufanya kazi ni adhabu iliyotokana na uasi uliofanywa na Adamu na Eva. Andiko letu hapo juu, halikubaliani na dhana hii. Baada ya Mungu kufanya kazi kwa siku sita, aliwataka wanadamu aliowaumba, nao wafuate nyayo zake kwa kufanya kazi. Mungu ni mchapa kazi, hivyo anahitaji kushirikiana na watu wanaofanya kazi kwa bidii.
Kwa kuwa Mungu hataki kushirikiana na mtu anayekaa katika hali ya kubweteka bila kufanya lo lote, alimpa Adamu na mkewe jukumu la Kuivalisha (‘abadar’ Heb) na kuiangalia (‘shamar’ Heb) bustani ya Edeni. Kuvisha na kuangalia kunakozungumziwa hapa, kunaweza kutafsiriwa kama kuiendeleza bustani hii hadi kujaza nchi ya Edeni. Kutokana na wajibu huu, mwamini ye yote asiye na wajibu wa kiroho na kimwili anaoufanya, huyo yuko nje ya mapenzi ya Mungu.
Ili kuupendeza moyo wa Mungu ni lazima mwamini awe na shughuli ya kiroho na kimwili anayoifanya ndani na nje ya kanisa. Pamoja na kuwa na shughuli ya kufanya katika eneo la kiroho na kimwili, anatakiwa aweke bidii kuzifanya shughuli hizo. Ukweli huu ndio unaomfanya mtume Paulo aliandikie kanisa la Thesalonike akisema, asiyefanya kazi, hata kula asile (2 Wathesalonike 3:10). Ingawa kazi iliyozungumziwa na mtume Paulo hapa ni ile inayompatia mtu mkate wa kila siku, bado agizo hili linagusa pia maeneo ya kiroho. Kuwa na tabia ya kushiriki baraka za kiroho zinazotolewa na huduma fulani bila kuchangia, ni kuwaibia wale wanaohusika kutegemeza huduma hiyo. Hivyo asiyetaka kujitolea katika ushirika unaomlea kiroho, anatakiwa asishiriki baraka za kiroho zinazotolewa na ushirika huo.
SHARTI LA KUISHI BUSTANINI
Sanjari na jukumu la kuiendeleza na kuitunza bustani ya Edeni, Mungu aliweka mti wa kujua mema na mabaya katikati ya bustani hiyo na kuwazuia wanadamu kula matunda yake. BWANA Mungu akamwagiza huyo mtu na kumwambia, “Uko huru kula matunda ya mti wo wote katika bustani, lakini kamwe usile matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, kwa maana siku utakapokula matunda yake, hakika utakufa” (Mwanzo 2:16-17). Huu ni ukweli wa pili tunaokutana nao pale tunapoingia katika agano na Mungu. Katika agano kuna wajibu kwa pande mbili zinazohusika katika agano na kuna masharti ya agano.
Mara zote upendo wa kweli unakuwa na masharti au mipaka isiyotakiwa kuvukwa. Kwa kumwekea Adamu na Eva mipaka wasiyotakiwa kuivuka, Mungu alikuwa anapanua wigo wao wa kuishi kwa uhuru. Kama kusingelikuwa na kitu kingine cha kupenda, ni wazi upendo wao usingelikuwa na nguvu kama vile ulivyotakiwa kuwa baada ya kuwekewa kitu kingine cha kuvuta upendo wao. Mara kwa mara nimewaambia watu kuwa, kama Eva angelikuwa na jicho moja peke yake upande wa kisogoni na wakati huo huo kusiwepo na mwanamke mwingine, bado Adamu angelimpenda. Hata hivyo upendo wake ungelikuwa ni ule wa kupenda, kutokana na kukosekana kwa mwanamke mwingine wa kupenda. Mungu yeye alikataa upendo wa aina hii, hivyo alimwewekea Adamu na Eva kitu kingine cha kuvuta upendo wao, yaani, matunda ya mti wa kujua mema na mabaya.
Hivi ndivyo ilivyo hata katika kipindi hiki cha Agano jipya, Mungu amelipatia kanisa mipaka ya neno lake isiyotakiwa kuvukwa. Kutovuka mipaka ya neno la Mungu ndilo sharti la agano kati ya Mungu na kanisa. Yeye hawezi kuvuka mipaka ya neno lake na mwanadamu naye, anatakiwa kutopungua au kuzidi kipimo cha neno la Mungu.
ANGUKO NA MAZINGIRA YAKE
Tunapoendelea na kipengele hiki, ni vema tutambue kuwa tunapozungumzia juu ya anguko la wanadamu wa kwanza, tunaongelea juu ya Adamu na Eva kwenda kinyume na masharti waliyopewa na Mungu, ya kuishi katika bustani ya Edeni. Kuhusu kishawishi kilichowaangusha wanadamu, Musa aliandikika maneno yafuatayo; Basi nyoka alikuwa mnyama mwerevu kuliko wanyama wote wa porini ambao BWANA Mungu aliwafanya. Nyoka akamwambia mwanamke, “Ati kweli Mungu alisema, Kamwe msile matunda ya mti wo wote bustanini?” (Mwanzo 3:1)..
Mwasisi wa anguko la mwanadamu
Ingawa kwa juu juu andiko tulilokwisha kulisoma linamwonyesha nyoka kama chanzo cha anguko la mwanadamu, mazingira ya uumbaji yanamfanya nyoka asiwe mwasisi wa mawazo yaliyowaangusha wanadamu. Nyoka alikuwa tu daraja la wazo baya, ila kiumbe mwingine alipita juu ya daraja hilo.
Ili mtu awe mwasisi wa ubaya utakaompata mtu mwingine, ni lazima yeye mwenyewe awe na ubaya ndani yake. Kama nyoka angelikuwa na ubaya ndani yake, ni wazi angelikuwa chanzo cha ubaya uliowaangusha wanadamu. Ila tunapoangalia uumbaji wa Mungu uliohusisha falme za vitu vyote venye uhai, hakuna mahali po pote tunaposoma kuhusu kuwepo kwa uovu au kasoro katika uumbaji huo. Tunachosoma katika maandiko ni kuwa, baada ya uumbaji Mungu aliangalia kazi za mikono yake, na kuona kuwa kila kitu ni chema sana. Mungu akatazama vyote alivyoumba na tazama vilikuwa vizuri sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi siku ya sita (Mwanzo 1:31).
Kwa kuwa anguko la Lusifa lilitokea kabla ya kuanguka kwa Adamu na Eva, yeye ndiye kiumbe pekee katika kipindi hicho, aliyekuwa na uovu ndani yake. Kutokana na ukweli huu, yeye ndiye aliyeweka wazo la uovu ndani ya ufahamu wa nyoka. Kwa kuwa Lusifa anamchukia Mungu, alitumia uovu aliokuwa nao kutengeneza mpango wa kumtenganisha Mungu na kipenzi chake (mwanadamu). Wakati muafaka ulipofika, aliliweka wazo hilo kwa nyoka.
Kinachoonekana katika andiko hili, ni kuwa Shetani alisikia maneno yote ambayo Mungu alimweleza Adamu na Eva, siku ile alipomweka katika bustani ya Edeni. Maneno haya yalihusu wajibu na masharti ya kuishi katika Edeni. Kwa kujua sharti hili, Shetani aliingiza mawazo kwa nyoka kwa lengo la kushawishi wanadamu kuvuka mipaka waliokatazwa kuivuka. Kutokana na ukweli huu, tunaweza kuona kuwa kabla ya kuteka ufahamu wa mwanamke, Shetani alitangulia kuteka ufahamu wa nyoka. Baada ya nyoka kukubaliana na mawazo yaliyokuwa kinyume na mapenzi ya Mungu, alikubali kuwa daraja la kuyafikisha mawazo hayo kwa mwanamke.
Ukweli mwingine unaoonekana hapa ni kuwa, miaka iliyotangulia kabla ya anguko, wanadamu walikuwa na uwezo wa kuwasiliana na wanyama kwa njia iliyo wazi. Baada ya anguko uwezo huo, ulitoweka. Hebu tumwombe Mungu atusaidie, kukataa kuwa daraja la kupitishia sumu itakayoharibu maisha ya wengine.
Kushawishika na kuanguka kwa mwanadamu
Mwanamke alipoona kuwa tunda la mti huo lilikuwa zuri kwa chakula na la kupendeza macho, tena linatamanika kwa kujipatia hekima, basi akachuma katika matunda yake, akala, pia akampa mumewe, aliyekuwa pamoja naye, naye akala (Mwanzo 3:6). Baada ya Shetani kufanikiwa kufikisha wazo lake kwa uzao wa wanadamu, Eva alianguka katika mtego uliomwangusha nyoka. Akiwa na akili timamu, alikubaliana na ushawishi ulio kinyume na mapenzi ya Mungu na kula matunda aliyokatazwa.
Mara zote Shetani hana uwezo wa kumlazimisha mtu kufanya kinyume na mapenzi ya Mungu. Kile anachofanya, ni kuingiza ushawishi mbaya ndani ya akili za watoto wa Mungu na kuwashawishi kuukubali. Kitakachozaliwa baadaye, kitategemea jinsi mwanadamu atakavyoufanyia kazi ushawishi huo. Kama ataamua kuwa kinyume nao, ataendelea kubakia katika mapenzi ya Mungu. Kinyume cha hapo, ataanguka na kuwa mbali na mapenzi ya Mungu. Adamu na mkewe, wao waliamua kutendea kazi mipango iliyopandikizwa na Shetani ndani yao. Ni jambo baya mno, kuelewa mapenzi ya Mungu na kwenda kinyume nayo. Nguvu ya ushawishi iliyotumiwa na Ibilisi kumwangusha Eva na kisha mumewe ilibeba mionjo ifuatayo:-
Kutokutosheka na mapenzi ya Mungu
Mwanamke alipoona kuwa tunda la mti huo lilikuwa zuri kwa chakula...(Mwanzo 3:6). Katika mambo lukuku yanayowatenganisha wanadamu na Mungu, kutokutosheka ni sababu ya kwanza katika orodha ya mambo hayo. Adamu na Eva waliruhusiwa kula matunda ya miti yote, ila tu walikatazwa matunda ya mti mmoja. Ni jambo lisiloingia akilini, kupewa kibali cha kula matunda ya miti yote iliyoko katika ulimwengu mzima na bado mtu atake kula matunda ya mti mmoja tu aliyozuiliwa kuyala.
Kuanguka kwa Adamu na Eva kunatufundisha kuridhika na yale Mungu anayotupatia katika maisha yetu. Sisi kama watoto wa Mungu hatutakiwi kutafuta mambo yaliyo ya ratiba ya Mungu. Yale tuliyo nayo, ndiyo Mungu aliyokusudia tuwe nayo, hivyo tusikubali kwenda kinyume na neno la Mungu, ili tupate yale tunayohisi kutokuwa nayo.
Kibarua cha kutumikia tumbo
Mwanamke alipoona kuwa tunda la mti huo lilikuwa zuri kwa chakula...(Mwanzo 3:6). Jambo la pili lililomfanya Eva akubaliane na ushawishi kutoka kwa Shetani, ni kibarua cha kulitumikia tumbo. Nakiita kibarua kutokana na ukweli kuwa, katika ulimwengu huu, hakuna kitu kinachodumu. Mwili pamoja na mambo mengi yanayotamanika kikiwemo chakula, mavazi, mapambo, anasa na starehe una mwisho wake.
Kibarua cha kutumikia tumbo ni kamba ya pili inayotumiwa na Shetani kuwanyongea watu wa Mungu. Wizi, zinaa, ujambazi, madawa ya kulevya, ufisadi, rushwa vyote hivi kwa kiwango kikubwa vinafanyika ili, kushibisha matumbo ya wanadamu. Eva alipoona kuwa matunda ya mti huo yalikuwa mazuri kwa chakula, alitwaa matunda hayo na kuyala. Tukijua kuwa tumbo pamoja na masumbufu yake ni vitu vya muda, ni vema tuseme hapana, pale tumbo linapotutoa nje ya mapenzi ya Mungu.
Tamaa mbaya ya macho
...na la kupendeza macho...(Mwanzo 3:6). Tamaa ya macho ni jambo lingine lililochangia kumshawishi Eva kuvuka mipaka aliyokatazwa na Mungu. Macho ni moja ya viungo vizuri vinavyoweza kumletea mwanadamu mafanikio makubwa pale vinapotumika vizuri. Asilimia kubwa ya uvumbuzi na utaalamu unaomzunguka mwanadamu, umesababishwa na macho. Sanjari na ukweli huu, asilimia kubwa ya uchafu na uharibifu unaomzunguka mwanadamu, umechangiwa na matumizi mabaya ya macho.
Hiki ndicho kilichotokea kwa Eva, alitumia macho yake vibaya na kula matunda aliyokatazwa na Mungu kuyala. Tamaa ya macho ilimwangusha Eva na tamaa hii ndiyo inayoongoza katika kuwapeleka watu Jehanamu. Wakati fulani mtu mmoja alimwendea Fanny Crossby yule mwanamke mwimbaji kipofu, na kumuuliza ikiwa angelipendelea Mungu afungue macho yake. Jibu la Fanny Crossby lilikuwa la kushangaza, “Hapana sitamani kuona, huenda nikipewa uwezo wa kuona, nitaona mambo yatakayoniondoa katika uwepo wa Mungu!” Ni kweli, matumizi mabaya ya macho, yalimtoa Eva katika uwepo wa Mungu.
Roho ya kiburi na majivuno
...Tena linatamanika kwa kujipatia hekima... (Mwanzo 3:6). Mara zote kiburi na majivuno huandamana na kutokutosheka. Ukiangalia katika sura zinazojulikana kama sura za uumbaji, utaona kuwa mwanadamu alikuwa ameumbwa kwa namna ya kushangaza. Sanjari na kuumbwa kwa namna ya kushangaza, Mungu aliweka pumzi yake ndani ya mwanadamu na kumpa mamlaka ya kusimamia kazi ya uumbaji wake. Cha kushangaza ni kuwa, pamoja na kutendewa mambo yote haya, bado Adamu na Eva hawakutosheka. Ingawa walikuwa na hekima kiasi cha kuelewana na wanyama, bado walitamani hekima nyingine inayotokana na kwenda kinyume na maagizo ya Mungu. Huu ni uongo mwingine wa Ibilisi, kutokana na ukweli kuwa, hakuna baraka, mafanikio au hekima inayotokana na kuasi njia za Mungu. Kwa kudanganywa na mionjo hii minne iliyounganishwa na Ibilisi na matunda ya mti wa kujua mema na mabaya, Adamu na Eva walikosea sharti la kuishi katika bustani ya Mungu.
Hali hii ya kiburi na majivuno inaonekana pia ndani ya hamu yao ya kutaka kufanana na Mungu. “Kwa maana Mungu anajua ya kuwa wakati mtakapoyala macho yenu yatafumbuliwa, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya” (Mwanzo 3:5). Kama tulivyojifunza katika somo la kwanza, Adamu na Eva waliumbwa kwa namna ya kushangaza sana. Kutokana na ukweli huu, kutamani nafasi inayozidi ile waliyopewa na Mungu, ni kujiinua na kujikweza.
Kupitia vishawishi hivi, Adamu na Eva wakavuka mipaka waliyokatazwa na Mungu kuivuka. Wakala matunda waliyokatazwa ya mti wa kujua mema na mabaya. Katika somo linalofuata, tutaangalia madhara yaliyotokana na anguko lao.
Maswali ya kupima ufahamu
- Kulikuwa na miti mingapi maalum katika bustani ya Edeni?
- Ni mnyama gani aliyemdanganya Eva akala matunda aliyokatazwa?
- Nani alikuwa chanzo cha anguko la wanadamu?
- Fanny crossby alikuwa nani?
- Baada ya kujiona wako uchi Adamu na Eva walifanya nini?
- Ni kiumbe yupi wa kwanza kumwasi Mungu?
- Taja mambo yaliyomvutia Eva kula matunda aliyokatazwa.
|