KUWASHINDA WAFUKIA VISIMA Na Askofu Rodrick MbwamboUtangulizi: Tunapoyaangalia maisha ya baba yetu wa imani Ibrahimu, kwa namna moja tunaweza kuona kuwa, yalikuwa tofauti na yale ya mtoto wake Isaka. Mara kwa mara mambo huwa hivi, kizazi cha kwanza cha wokovu, kinakuwa na msimamo zaidi katika Mungu, kuliko kizazi cha pili na kuendelea. Pengo la kiroho kati ya kizazi kimoja cha kiroho na kingine, linaweza lisiwepo pale kasi ya yule anayepokea kijiti, inapokuwa kubwa kuliko ya yule aliyemkabidhi kijiti hicho. Kama kasi ya aliyekabidhiwa kijiti itapungua au kufanana na ile ya aliyemkabidhi kijiti, ni wazi matunda ya wakimbiaji hawa, itatofautiana. Utofauti wa mababa hawa wa Israeli, unaonekana katika ushindi ambao maadui waliupata katika kuvifukia visima ambavyo Isaka, aliachiwa na baba yake. Wafukia visima hawa walikuwepo pia wakati wa Ibrahimu, ila miaka hiyo, walishindwa kabisa kuyachezea maisha ya Ibrahimu. Hata pale maadui walipomvamia mjomba wake (Lutu), yeye aliingia vitani na kumrejesha Lutu pamoja na mali zake. Mambo yalionekana kubadilika, mara tu baada ya kifo cha shujaa huyu wa imani. Kama ilivyokuwa kwa Sulemani baada ya kifo cha Daudi, ndivyo ilivyokuwa kwa Isaka. Baada ya kifo cha baba yake, maadui walifanikiwa kuvifukia visima alivyoachiwa kama urithi, kumfukuza katika makazi yake ya awali na kumnyang’anya visima vilivyochimbwa na watumishi wake. Mwanzo 26:15 Kama ilivyokuwa wakati wa Ibrahimu na Isaka, wafukia visima tunao katika maisha yetu ya kila siku. Visima wanavyolenga kuvifukia ni pamoja na maisha ya waamini ya kulitii neno la Mungu, amani katika ndoa, upenyo wa kibiashara, kupanda daraja kazini, ushindi katika masomo, afya na kadhalika. Kama vile ilivyotokea kwa Isaka na Ibrahimu, uko uwezekano wa kushindwa au kuwashinda Wafukia visima. Ili kuwashinda Wafukia visima na wanyang’anya visima wa siku zetu, tunatakiwa kuungana na Ibrahimu kufanya yale yaliyompatia ushindi wakati wa uhai wake. Mambo yaliyompatia ushindi ni pamoja na haya yafuatayo :- KUMTII MUNGU KATIKA YOTE
“BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha….Basi Abramu akaenda, kama BWANA alivyomwamuru.” Mwanzo 12:2-3 Jambo la kwanza lililochangia katika kumpatia Ibrahimu ushindi, ni kiwango chake cha kumtii Mungu. Kibinadamu, halikuwa jambo rahisi kwake kuacha maskani yake ya awali na kwenda kuishi katika nchi nyingine asiyoijua. Pamoja na ugumu uliokuwepo, bado Ibrahimu aliamua kumtii Mungu kuliko kuutii mwili wake. Utii wa Ibrahimu unaonekana pia, pale alipopata mtihani wa kumtoa mwanawe wa pekee kama dhabihu kwa ajili ya Bwana. Kitendo cha kumchinja mtoto juu ya madhabahu na baadaye kumteketeza kwa moto nacho kilibeba ugumu usiopimika kwa mizani wala shubiri. Ila pamoja na ugumu huu, Ibrahimu alifanya sawasawa na maagizo yote ya Mungu. Mwanzo 22:2-6 Kwa yeyote anayetaka kuwashinda wafukia visima, maisha yake yanatakiwa kusimamia nguzo hii ya utii. Katika hili, ni vema tutambue kuwa, kamwe haiwezekani kumtii Mungu asiyeonekana na wakati huo huo, kutowatii wale wanaotuongoza kiroho na kimwili. Neno la Mungu linapoelezea uhusiano uliopo kati ya yale tunawafanyiayo wengine dhidi ya Mungu, imetumia andiko lifuatalo:- “ Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye anamwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona.” 1 Yohana 4:30. Andiko hili linatuonyesha wazi kuwa, kama tunahitaji kuyaona matunda ya utii, ni lazima utii huo uanzie kwa viongozi wetu wa kiroho na kimwili tunaoishi nao. Kama ni watoto, waonyeshe utii kwa wazazi wao, wanafunzi kwa waalimu wao, waajiriwa kwa wakuu wao wa kazi, waamini kwa wachungaji wao na kadhalika. Hata hivyo, utii huu, unatakiwa uwe katika yale tu yaliyo sawasawa na neno la Mungu. Sambamba na kuwatii wanadamu, tunatakiwa pia kumtii Mungu kupitia kulitii neno lake, pamoja na kumtii Roho Mtakatifu. KUJENGA MADHABAHU (mizbayakn-kiebrania)
“Kisha akaondoka huko, akaenda mpaka mlima ule upande wa mashariki wa Betheli, na Ai upande wa mashariki; akamjengea BWANA madhabahu huko, akaliitia jina la BWANA.” Mwanzo 12:8 Siri nyingine iliyomfanikisha Ibrahimu kuwashinda Wafukia visima, ni ile tabia yake ya kumjengea Mungu madhabahu. Tunapoyaangalia maisha ya shujaa huyu, tunaona kuwa, kila mahali alipokwenda, alimjengea Mungu madhabahu. Mwanzo 13:4, 18; 12:7; 22:9. Ujengaji huu wa madhabahu, unawakilisha mambo makubwa matatu. Jambo la kwanza, ujenzi wa madhabahu, unasimama badala ya maisha ya utakatifu au dhamira kuutafuta uso wa Mungu. Huu ni ukweli ulio wazi kuwa, yule anayeingia katika tabu ya kumjengea Mungu madhabahu, ni mtu aliyeamua kuishi maisha ya kumpendeza Mungu. Mtu asiye na haja na Mungu, huyo hatahangaika kukusanya mawe ili kumjengea Mungu madhabahu. Ujenzi wa madhabahu, unawakilisha pia huduma ya UTOAJI, katika maeneo makubwa matatu. Kwanza, ni ule utoaji unaozihusu nguvu alizojaliwa mtu kuwa nazo. Utoaji huu unawakilishwa na zoezi zima la kukusanya mawe na kujenga madhabahu. Sehemu ya pili ya utoaji katika kumjengea Mungu madhabahu, inahusu utoaji wa ujuzi na vipawa. Baada ya mhusika kutumia nguvu kukusanya mawe, zoezi linalobakia ni kutumia ujuzi na vipawa vyake kuumba umbo la madhabahu kwa kutumia mawe hayo. Kile ninachotaka ukione hapa ni kuwa, ulihitajika ujuzi katika kumjengea Mungu madhabahu. Sehemu ya tatu ya utoaji inayoonekana katika huduma ya kumjengea Mungu madhabahu, ni ile ya mhusika kutoa mali zake kwa ajili ya Mungu, aliyemjengea madhabahu hiyo. Maandiko yanapoielezea hatua hii ya utoaji, ilikuwa na haya ya kusema, “Wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhabahu huko, akaziweka tayari kuni, kisha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka juu ya madhabahu, juu ya zile kuni. “ Mwanzo 22:9. Nafasi ya utoaji katika kumjengea Mungu madhabahu, inaonyesha vile maisha ya Ibrahimu yalivyosimamia nguzo ya kujitolea kwa hali na mali. Kwa kujitoa huku, Mungu alimheshimu na kumpa kushinda kila alipokwenda. Kama kanisa la siku hizi za mwisho, linataka lione ushindi wa Mungu katika kutumika kwake, linatakiwa kuweka bidii katika kumtumikia Mungu kwa hali na mali. Jambo la tatu katika kumjengea Mungu madhabahu, linahusu maombi na kuabudu. Mara zote dhabihu inapoteketea juu ya madhabahu, huo ndio wakati mzuri kwa mtoaji kukunjua mikono yake mbele za Mungu. Katika kufanya hivi, mwamini atamwambia Mungu haja zake pamoja na kumwabudu. Ukweli huu unatuonyesha kuwa, sambamba na Ibrahimu kuuishia utakatifu pamoja na utoaji, alikuwa pia mtu wa maombi na kuabudu. Kama tunahitaji kuwa mabwana dhidi ya maadui zetu, ni lazima tuvishinde vishawishi vyote vinavyotuzuia kuomba na kumwabudu Mungu. Ili kuielewa huduma hii ya kuomba kwa undani, soma kitabu kilichoandikwa na Askofu Rodrick Mbwambo kiitwacho, HUDUMA YENYE THAWABU ukrasa wa 19-40. KUYAFANYA MAPENZI YA MUNGU “Basi Abramu akaenda, kama BWANA Alivyomwamuru.” Mwanzo 12:6 Moja ya mambo yanayonyonya utakatifu na nguvu ya Mungu katika kanisa la leo, ni ile tabia ya waamini kufanya mambo tofauti kabisa na vile maagizo yalivyo. Maagizo yanaweza kuwa wazi kama maji, na bado waamini wakafanya kinyume kabisa na maagizo hayo. Sisi kama kanisa la siku za mwisho, ni lazima tutambue kuwa, tumeokolewa ili tuyafanye mapenzi ya Mungu badala ya kufanya mapenzi yetu. Kama Mungu angelitaka tuishi kwa kuongozwa na mapenzi yetu, kusingelikuwa na sababu ya yeye kuileta Biblia katika Ulimwengu. Biblia iliandikwa ili kuwapa waamini nafasi ya kuyajua mapenzi ya Mungu na kuyafanya. Ibrahimu aliujua ukweli huu kivitendo, pale alipohakikisha kuwa, anafanya sawasawa na vile alivyoagiza kufanya. Alipoagizwa kukubaliana na mkewe kumwondoa mjakazi na mtoto wake, alifanya hivyo; hali kadhalika alipoambia jambo gumu la kumtoa mwanawe kuwa kafara, hakuchelea kufanya hivyo. Mwanzo 22:1-10 KUWA MWAMINI WA MITEGO MINGI
“Abramu akarudi kutoka kumpiga Kedorlaoma na wale wafalme waliokuwa pamoja naye, mfalme wa Sodoma akatoka amlaki katika bonde la Shawe, nalo ni bonde la Mfalme.” Mwanzo 14:17 Jambo lingine lililochangia kumfanya Ibrahimu kuwa tishio kwa watesi wake, ni ule utayari aliokuwa nao kufanya huduma zaidi ya moja. Katika andiko letu hapo juu, tunaona kuwa, sambamba na kujenga madhabahu, shujaa huyu, alikuwa pia mpiganaji. Hali kadhalika, yako maandiko yanayomwelezea kama mchimba visima. Moyo huu wa kuwa tayari kufanya huduma yoyote ya kiroho au ya kimwili itakayomletea Mungu utukufu, ni tabia iliyo adimu sana katika kanisa la siku hizi za mwisho. Leo hii watumishi na waamini wengi wanachagua la kufanya katika nyumba ya Mungu, badala ya kuwa tayari kujishughulisha na tatizo lolote lile, litakalojitokeza katika nyumba ya Mungu. Hali hii ndiyo inayowafanya baadhi ya waamini kujisaidia katika vyoo vichafu kanisani na kuviacha katika uchafu huo, bila kuvisafisha. Hali kadhalika, wako wale wanaopita takataka katika uwanja wa kanisa bila kuinama na kuziokota takataka hizo. Kama wewe ni mwamini unayetaka kuuona ushindi aliouona Ibrahimu katika maisha yake, ni vema uhakikishe kuwa, unakuwa tayari kutatua tatizo lolote lile, litakalojitokeza katika nyumba ya Mungu. Kama umeitwa kutumika katika ofisi ya kitume, kinabii, kiinjilisti, kichungaji au ualimu, bado unaweza kusafisha choo cha kanisa, kunyweshea maua, kufagia uwanja wa kanisa, kufundisha watoto wadogo na huduma zingine zinazofanana na hizi ndani na nje ya kanisa. Hali hii ya kuwa na mitego mingi, inatakiwa iguse pia maisha ya kila siku ya kimwili. Kamwe mtu hawezi kufanikiwa kwa kutembeza kilo moja ya karanga kwa siku, bali, sambamba na kuuza njugu, anaweza pia kuuza bisi. Kama biashara ni ya vitumbua, anaweza kuongeza pia kwa kuuza chapati, madazi au supu. Kwa wale walioajiriwa, wanaweza kutumia muda wa ziada kufanya biashara fulani inayotoka nyakati za usiku. Mara zote mwamini aliye tayari kufanya zaidi ya huduma moja katika maisha yake ya kiroho au kimwili, huyo atavuta wingi wa mafanikio, kuliko yule aliyejifungia katika huduma moja. KUISHI MAISHA YA KUGHARIMIA“Akamwambia Efroni, na watu wa nchi wanasikiliza, akisema, Tafadhali unisikilize; nitatoa kima cha shamba, nawe ukipokee kwangu, nami nitamzika humo maiti wangu. Efroni akamjibu Ibrahimu, akamwambia, Bwana wangu, unisikilize. Sehemu ya nchi, ambayo thamani yake ni shekeli za fedha mia nne…Ibrahimu akampimia Efroni ile fedha aliyotaja masikioni mwa watu wa Hethi.” Mwanzo 23:12-16 Andiko letu hapo juu, linaonyesha jambo lingine lililompatia Ibrahim heshima na kuufanya utisho wa Mungu uandamane naye kila mahali anapokwenda. Sura hii ya 23, ilianza kwa ombi la Ibrahimu kwa watu wa Hethi, kumpatia eneo kwa ajili ya kuzika mwili wa Sara. Baada ya ombi hili, watu wa Hethi walikubali kutoa eneo hili bure kwa ajili ya Ibrahimu. Kwa waamini wengi wa siku hizi za ‘dezo’, jambo hili lingehesabika kama muujiza, ila Ibrahimu alipotazama upande wa pili wa dezo, aliweza kukataa ukarimu huu. Watu wengi waliofanyia utafiti maswala ya bure katika jamii, wamegundua kuwa, mara nyingi vitu vya bure au vilivyo nafuu, baadaye huwa na gharama kubwa zaidi ya vile ambavyo mtu, angelivigharimia! Ukweli huu, ndio uliomfanya, Ibrahimu aamue kuligharimia eneo hili, badala ya kulipokea bure. Unafahamu katika miaka tuliyo nayo, roho ya kujitolea na kugharimia, imekuwa adimu sana ndani na nje ya mwili wa Kristo. Miaka ya kale, inayohesabika kuwa mibaya kiuchumi, watu waliweza kujitolea kuchimba mabarabara, kujenga makanisa makubwa, kujenga mashule na kujenga mahospitali. Leo badala ya watu kujitolea katika mambo ya jinsi hii, wanaishia kuomba na kufunga ili Mungu alete wafadhili wa kufadhili mambo haya. Katika baadhi ya makanisa, idadi ya waamini wanaotaka kuyaona mafanikio ya kiroho na kimwili kwa kugharimia ni chini ya asilimia 20. Hali hii ya kutokuwa tayari kugharimia, kwa upande mwingine imeyageuza maombi ya watumishi wa Mungu kuwa kama chombo cha ushirikina. Katika miaka hii, ni rahisi kuwaona waamini wasio na shughuli yoyote ndani na nje ya mwili wa Kristo, wakiwa kwenye mlolongo wa watu wanataka kuombewa ili wapate upako na baraka za kimwili kama vile magari, majumba na kadhalika. Hali hii imezaa pia watumishi wanaozurura katika majumba na maofisi ya watu, wakiomba misaada ya kifedha ili kuyaendesha maisha yao na familia zao! Kutokana na roho hii ya kupenda dezo, badala ya kanisa la Mungu kuwa ushirika ulio na majibu, jamii inaliona kama genge la wazururaji linalotafuta majibu kutoka kwa watu wanaojishughulisha! Ibrahimu yeye hakuwa hivyo. Badala ya kungojea kutafuniwa ndipo ameze, alimwambia Efroni kuwa, atatoa kiasi cha pesa kinacholingana na shamba analolihitaji kwa ajili ya kuzikia. Roho hii ya kugharimia, ndiyo iliyomfanya kuwa tishio kwa wafukia visima. Kama kanisa la sasa linahitaji kuishi maisha ya ushindi, ni lazima likubali kugharimika. T.L.Osborn, alisema wakati fulani kuwa, “mtu anayekwepa bajeti kubwa, huyo ataishia kufanya mambo madogo!” Katika hili, si kwamba tunakataa roho ya kusaidiana kwa kuwa, muda nchi idumupo, kusaidiana kutaendelea kuwa nguzo muhimu katika kusukuma mbele maendeleo ya watu ndani na nje ya kanisa. Kile tunachokikataa hapa ni ile hali ya kubweteka na kutegemea kuendelezwa na watu wengine wanaojishughulisha. KUTUMAINI KUWEZESHWA NA MUNGU“Mfalme wa Sodoma akamwambia Abramu, Nipe mimi hao watu, na hizo mali uchukue wewe. Abramu akamwambia mfalme wa Sodoma, Nimeinua mkono wangu kwa BWANA, Mungu aliye juu sana, Muumba wa mbingu na nchi, ya kuwa sitatwaa uzi wala gidamu ya kiatu wala chochote kilicho chako, usije ukasema, Nimemtajirisha Abramu.” Mwanzo 14:21-23 Maandiko mara nyingi yametamka wazi kuwa amelaaniwa mtu anayeruhusu nafasi ya Mungu katika maisha yake, ichukuliwe na mwanadamu. Yeremia 17:5. Tunapoangalia maisha ya Ibrahimu tunaweza kuona kuwa ingawa alikuwa ni mtu wa watu, kamwe hakuruhusu wanadamu wachukue nafasi ya Mungu katika maisha yake. Alifahamu fika kuwa, Mungu ndiye aliyemwita na Yeye ndiye atakayeifanikisha njia yake. Ukweli huu, ndio uliomfanya akatae nyara alizopewa na mfalme wa Sodoma. Alikataa nyara hizo huku akisema, ”Sitaki atokee mtu wa kusema kuwa, amemtajirisha Abramu!” Usemi huu ni adimu sana katika kizazi tulicho nacho kinachotaka utajiri na mafanikio ya kimwili, bila kujali kule yalikotokea. Hali ya kumwangalia mwanadamu badala ya kumwangalia Mungu, ndiyo inayowapeleka waamini wengi katika hatua ya kuwaabudu wanadamu badala ya kumwabudu Mungu. Katika hili ni rahisi kuwaona waamini, wakitafuta kukaa karibu na watu waliofanikiwa ili waambulie chochote kwao, badala ya kupigania kukaa karibu na Mungu. Hali hii ndiyo pia inayowafanya waamini wengi kupenda kusoma historia badala ya kuandika historia. Mwamini anaona kanisa lililofanikiwa kihali na mali, na anaamua kutoka katika kanisa lake dogo la nyasi na kujiunga na kanisa hilo la kifahari. Hapa sipingi uhuru wa mtu kujiunga na ushirika anaovutiwa nao, ila kama mwamini atangojea wengine wataabike na yeye aje tu ‘kujinoma’, huo ndio unajisi usiotakiwa. Kama tunahitaji kuishi maisha ya ushindi, ni lazima tutambue kuwa, Mungu ndiye aliyetuumba kama wanadamu na yeye ndiye atakayetufanya tuishi sawasawa na mapenzi yake. Katika hatua yoyote ya maisha, kama ni ya uanafunzi, kuajiriwa, biashara au kuhudumia roho za watu, tutambue kuwa, Mungu atatufanikisha. Ibrahimu, alitembea katika ukweli huu na kuamini kuwa, Mungu aliyemwita, ndiye atakayemtoa katika maisha ya uchache na kumpeleka katika maisha aliyomkusudia. KUWATANGULIZA WENGINE“Kukawako ugomvi kati ya wachunga wanyama wa Abramu, na wachunga wanyama wa Lutu; Na siku zile Wakanaani na Waperizi walikuwa wakikaa katika nchi. Abramu akamwambia Lutu, Basi, usiwepo ugomvi, nakusihi, kati ya mimi na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wachungaji wako; maana sisi tu ndugu. Je! nchi yote hii haiko mbele zako? basi ujitenge nami, nakusihi; ukienda upande wa kushoto, nitaenda upande wa kulia; ukienda upande wa kulia nitaenda upande wa kushoto...Basi Lutu akachagua bonde lote la Yordani.” Mwanzo 13:7-11 Tabia nyingine ilichangia kumjengea Ibrahimu jina, ni hii ya kuwatanguliza wengine, katika mambo ya heri. Katika ulimwengu tulio nao, roho hii ya kutangulizana katika mema imekuwa adimu sana. Kama hali hii ya kuwatanguliza wengine itatokea, mara nyingi itakuwa katika mambo yasiyo na neema ndani yake. Kuhusu vile wanadamu walivyoweza kuwatanguliza katika mambo ya shari, nina mfano ulio hai uliotokea katika nchi moja katika bara la Afrika. Katika mji mmoja kulikuwa na ndugu aliyekuwa katika mgogoro na mwenzake kuhusiana na biashara haramu waliyoifanya pamoja. Baada ya miaka mingi ya kulumbana na kudaiana, mdaiwa alimwagiza mdai wake aende mahala fulani na huko atawatuma watu wamletee mdai kilicho chake. Baada ya mdai kufika katika eneo walipopatana akiwa na gari ya kukodi, alianza kushambuliwa na wazo la kuuawa badala ya kupewa pesa. Ili kujionea ukweli wa mambo, alijifanya kuwa ameshikwa na haja, hivyo akamwomba dereva kubakia pale na yeye akaenda upande mwingine wa pori. Akiwa upande mwingine wa pori, alichungulia ili kuona kile kitakachotokea pale waliotumwa na mdaiwa wake watakapofika. Kweli baada ya muda mfupi, watu hao walikuja na walipomwona yule dereva, walianza kummiminia risasi wakidhania kuwa ndiye mdai. Baada ya kushuhudia mauaji hayo ya kutisha, mdai aliondoka katika pori lile, huku akiuacha mwili wa yule dereva ukiwa umelala katika manyasi! Ibrahimu, alifanya kinyume kabisa na kile kilichofanywa na ndugu huyu, yeye aliwatanguliza wengine katika mambo heri. Alifanya hivyo pale alipomwachia mfalme wa Sodoma nyara zote walizozipata vitani na pia, alifanya hivyo kwa Lutu pale wachungaji wa mifugo yao, walipogombania malisho. Yeye kama kiongozi wa familia iliyomjumuisha Lutu, alikuwa na haki ya kuchagua eneo na kisha kumwambia Lutu aende eneo lingine. Kama angelifanya hivi, isingelikuwa dhambi, ila alichagua kutofanya hivyo. Kuonyesha vile baraka zinavyoweza kumjia mtu pale, anapoisahau nafsi yake na kuwatanguliza wengine, baada ya kumtanguliza Lutu, Mungu alikuwa na haya ya kumwambia:- “Inua sasa macho yako, ukatazame kutoka hapo ulipo, upande wa kaskazini, na wa kusini na wa mashariki na wa magharibi; maana nchi yote hii uionayo, nitakupa wewe na uzao wako hata milele, Na uzao wako nitaufanya uwe kama mavumbi ya nchi, hata mtu akiweza kuyahesabu mavumbi ya nchi, na uzao wako nao utahesabika. Ondoka, ukatembee katika nchi hii, katika mapana yake, na marefu yake, maana nitakupa wewe nchi hiyo.” Mwanzo 13: 14-17 Kama tunahitaji kuwashinda maadui wanaofukia visima vya kiroho na kiuchumi katika maisha yetu ya kila siku, ni lazima sisi, tuwatanguliza wengine katika mambo yote yaliyo na heri ndani yake. Roho hii ya kuwatanguliza wengine, tunaiona pia kwa kuiangalia historia ya mama Corie Ten Boon. Mama huyu wa Kiholanzi pamoja na familia yake, walikuwa miongoni mwa maelfu ya watu waliotupwa gerezani, wakati wa mateso yaliyoongozwa na dikteta Adolf Hitler. Kazi katika magereza hayo zilikuwa ngumu sana, huku chakula walichopewa kikiwa kidogo na kibaya sana. Baada ya kazi ngumu, wafungwa walipewa supu nyepesi na kipande kikavu cha mkate ili kuwafanya tu waendelee kupumua. Pamoja na njaa kali aliyokuwa nayo baada ya kazi ngumu, mara kwa mara Corie, aligawa supu na mkate wake kwa wamama waliokuwa wagonjwa na yeye akalalia kumeza mate! KUISHI MAISHA YA UTOAJI “Malaika wa BWANA akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni, akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema BWANA, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kukubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.” Mwanzo 22:15-18 Andiko letu hapo juu, linatuonyesha kuwa utoaji, ni jambo lingine lililomwezesha Ibrahimu kuwashinda wale wote waliokuwa kinyume na kufanikiwa kwake. Ingawa aliishi kabla ya agano jipya, kupitia andiko hili, tunaona kuwa, aliishi sawasawa na lile andiko la dhahabu linalosema kuwa; “ni heri kutoa kuliko kupokea.” Matendo 20:35. Kama tulivyotangulia kuona katika vipengele vilivyotangulia, utoaji wa Shujaa huyu, unaonekana katika zoezi zima alilokuwa akiliendesha la kumjengea Mungu madhabahu. Kupitia ujenzi huu wa madhabahu, Ibrahimu aliweza kumtolea Mungu nguvu zake, ujuzi wake, mali zake pamoja na maombi. Mwanzo 18:1-8; 22:1-9. Tunapowaangalia waamini wa kanisa la siku hizi za mwisho, tunaweza kuona kuwa wengi wao, ni wale wanaoishi kinyume na roho hii ya utoaji. Neno la Mungu linasema kuwa, ni heri kutoa kuliko kupokea; wao wanasema ni heri kupokea kuliko kutoa! Kama kanisa la Kristo la kizazi chetu litaweka bidii kuyatendea kazi mambo haya yaliyochangia kuyainua maisha ya Ibrahimu, ni wazi Mungu ataliinua na kulitumia kwa namna isiyo ya kawaida katika siku hizi za ‘lala salama’. AMENI!
|
|---|