ZAIDI ya watu 100,000 wa kike na kiume, humpokea Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wao ulimwenguni kila siku. Nawe unaweza kujiunga na watu hawa kupitia hatua zifuatazo:-
TAMBUA KUWA U MWENYE DHAMBI
Neno la Mungu katika Warumi, linasema kuwa, “wanadamu wote wamefanya dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu.” Warumi 3:23
TAMBUA KUWA HUWEZI KUJIOKOA MWENYEWE
Mtume Paulo alipokuwa akielezea vile mwanadamu asivyoweza kuushinda dhambi kwa nguvu zake mwenyewe, alikuwa na haya ya kusema, “Lile nitakalo kulitenda silitendi na lile nisilotaka kulifanya ndilo ninalolitenda, nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?” Warumi 7:24
YESU ALIKUJA DUNIANI AKUOKOE
Akielewa jinsi wanadamu wasivyo na uwezo wa kuzishinda tamaa za mwili kwa nguvu zao wenyewe, nafsi moja ya Mungu ilichukua mwili wa kibinadamu na kuja duniani ili kuinyang’anya dhambi utawala. Ukweli huu umebebwa na andiko lifuatalo; “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa mwana wake wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele.” Yohana 3:16
DAMU YA YESU IMEIVUNJA NGUVU YA DHAMBI
Kabla ya ujio wa Yesu Kristo duniani, wanadamu wa vizazi vyote, walichinja wanyama, ili damu ya wanyama hao, iweze kuwapa kibali mbele za Mungu. Habili, Nuhu, Ibrahimu, Isaka, Yakobo, Musa na manabii wengine waliotanguliwa, walimwendea Mungu kupitia njia ya damu ya wanyama.
Kusulubiwa kwa Yesu Kristo juu ya msalaba zaidi ya miaka 2000 iliyopita, kulimaliza kipindi cha kumkaribia Mungu kwa njia ya damu ya wanyama. Kukamilika kwa kipindi hiki, kulifungulia mlango kipindi kingine cha milele cha kumkaribia Mungu kwa njia ya damu ya Yesu Kristo. Uwezo wa damu ya Yesu katika kumleta mwanadamu karibu na Mungu, ndio uliozaa andiko lifuatalo: “ Pasipo damu hakuna ondoleo la dhambi.”
RUHUSU DAMU YA YESU IINGIE NDANI YAKO
Kwa imani unaweza kumruhusu Mungu akusafishe kwa kutumia damu ya Yesu, pale utakapoomba sala ifuatayo kwa kumaanisha. Omba hivi:-
“Mungu Baba wa Bwana wangu Yesu Kristo, Ninaomba unisamehe dhambi zangu zote nilizofanya kwa kuwaza na kwa kunena na kwa kutenda. Futa jina langu katika kitabu cha hukumu na uliandike upya katika kitabu cha uzima cha Mwanakondoo. Ninaomba pia unipe nguvu za Roho wako Mtakatifu, ili anisaidia katika kukutafuata na kukushikilia kwa gharama yoyote ile. Ninaamini kuwa umenisikia na sasa nimefanyika mtoto katika familia yako. Ameni”
KWA KUWA SASA UMEOKOKA!
Wasiliana nasi ili tukupe maandiko yatakayokusaidia kuendelea na safari hii ya wokovu. Unapowasiliana nasi, tunaweza pia kukuelekeza jinsi ya kupata familia ya kiroho inayoweza kukulea kiroho. Wakati unapoyafanya haya yote, jenga tabia ya kuomba, kusoma Biblia takatifu na kuwaeleza wengine juu ya tumaini jipya ulilolipata kupitia uamuzi ulioufanya wa kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako.
|