KUELEA KWA CHUMA

Na Askofu Rodrick Mbwambo

Utangulizi:

Mara zote maisha ya wokovu, ni maisha ya mapambano makali, dhidi ya Ibilisi na jeshi lake. Mapambano haya ndiyo yanayowafanya baadhi ya watoto wa Mungu, kuishi kinyume na vile Mungu alivyowakusudia kuishi. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa, viko vitu vingi vilivyopaswa kuwa mikononi mwa watoto wa Mungu, ila Ibilisi amevipokonya na kuvizamisha majini. Kwa baadhi ya watoto wa Mungu, kilichozamishwa majini, ni baraka zao za kifedha, wengine ni afya, amani katika ndoa, mafanikio katika masomo na mambo mengine yanayofanana na haya. Hali hii ya kuponyokwa na kitu kikazama majini, ndiyo iliyompata mwanafunzi mmoja katika chuo cha manabii kilichokuwa kikiongozwa na Elisha.

Mwanafunzi huyu alikuwa ameazima shoka na wakati wa kukata mti, kichwa cha shoka hilo, kikachomoka na kuzama katika mto wa Yordani. Asante Mungu maana katikati ya huzuni yake, nguvu ya Mungu ilikibandua chuma hicho matopeni na kwa nguvu za Mungu, kikaelea majini! Kupitia andiko hili, tunajifunza vile ukuu wa Mungu ulivyo. Yeye anaweza kukusaidia hata pale adui anapokuwa amezamisha sehemu ya maisha yako katika maji na kukuachia mpini usio na shoka. Mungu yule aliyefanya chuma kielee wakati wa Elisha, anao uwezo wa kuifanya sehemu hiyo ya maisha iliyozama kuelea na kuijia mikono yako. Unachotakiwa kufanya, ni kufuatana nami katika somo hili lijulikanalo kama “kuelea kwa shoka.”


WAZO LA KUZAA KUELEA KWA CHUMA

“Kisha wana wa manabii wakamwambia Elisha, angalia basi mahali tukaapo mbele yako ni padogo kwetu. Basi twende mpaka Yordan, twakuomba, tutwae huko kila mtu mti mmoja, ili tujifanyie huko mahali pa kukaa.” 2 Wafalme 6:1-2

Miaka ya hivi karibuni umezuka mtindo katika timu kubwa za mpira, wa kumwenzi yule anayefanikiwa kuzitikisa nyavu za adui. Pamoja na nia nzuri waliyo nayo wale waliouanzisha utaratibu huu, utaratibu huu una kasoro kwa kuwa, unaangalia tu pale goli lilipoingilia na kusahau kule lilikotokea. Uko ukweli usiopingika kuwa, kazi kubwa ni ile iliyofanyika kabla ya mpira kuingia wavuni na wala sio ile ya kuuingiza mpira huo wavuni.

Hivi ndivyo inavyotokea pale muujiza unapofanyika. Kila mara muujiza unapotokea, watu huiangalia ile sekunde ya mwisho ya muujiza na kusahau mazingira yaliyouzaa muujiza huo. Mfano ulio hai tunaweza kuuona kwa kuuangalia muujiza huu wa kuelea kwa shoka. Kamwe muujiza huu usingelitokea kama kusingelikuwa na wazo kutoka kwa wana wa manabii la kupanua maskani yao. Ni katika harakati za kulitendea kazi wazo hili, ndipo mmoja wao alipoazima shoka, ambalo baadaye, lilichomoka na kuzama majini.

Hivi ndivyo inavyotakiwa kuwa kwa yule anayetaka kuona chuma cha shoka kikielea katika maisha yake. Kama chuma anachotaka kukiona kikielea ni cha mafanikio kiuchumi, uhusiano, afya, masomo, kiu ya maombi, bidii ya kuwaleta watu kwa Bwana au afya, ni lazima liwepo wazo au neno litakalouzaa muujiza huo. Kwa maneno mengine, mtu anayehitaji kuliona shoka likielea katika maisha yake, anatakiwa atambue kuwa, muujiza wowote ule, ni lazima uzaliwe na wazo au neno fulani la kimaendeleo.

Katika muujiza huu, wazo lilizaliwa kutokana na ufinyu wa mahali palipotumiwa na wana wa manabii kama maskani yao. Hali hii ya ufinyu wa mahali, ulikiumbia chuo cha manabii kiu na wazo la kuwa na sehemu kubwa zaidi. Katika hili tunaweza kuona kuwa, si wazo tu linalohitajika, ila wazo hilo ni lazima liwe lile linalomwondoa mtu katika hali iliyo duni kwenda katika hali ya neema. Kama mtu ataridhika na kukubaliana na upungufu unaoyasonga maisha yake, wazo la kimaendeleo halitakuwepo, hali kadhalika chuma cha shoka hakitaelea katika maisha yake. Hiki ndicho kilichofanywa na kundi la manabii wakati wa Elisha, walikataa kuminyana katika eneo dogo wakati uwezekano ulikuwepo wa kupata eneo lililo kubwa zaidi. Kama wangeliridhika na eneo hilo dogo, ni wazi wasingelikuwa na wazo hilo na muujiza wa kuelea kwa shoka usingeliweza kutokea.


KUANDAMANA NA UONGOZI

“Mmoja wao akasema, Uwe radhi, basi nakusihi, uende pamoja na watumishi wako.” 2 Wafalme 6:3

Jambo lingine lililochangia katika muujiza huu wa kuelea kwa shoka, ni ombi la mmoja wa wana wa manabii la kutaka kuandamana na kiongozi wao katika safari ile ya kukata miti. Hapa tena unaweza kuona kuwa, kama ombi hili lisingelitolewa, Elisha asingelikwenda pamoja nao, na muujiza huu mkubwa, usingelitokea. Ombi hili la mwana wa nabii limebeba kweli kadhaa zilizochangia kukifanya chuma kielee.


Upendo kwa kiongozi na anaowaongoza

…Uwe radhi, basi nakusihi, uende pamoja na watumishi wako.” 2 Wafalme 6:3

Wana hawa wa manabii walimpenda kiongozi wao, kiasi cha kutaka kuandamana naye kila mahali walipokwenda. Kama upendo huu usingelikuwepo, ni wazi wasingelimwomba ili aandamane nao. Mara nyingi waamini wengi wamekosa kuziona baraka za Bwana  katika maisha yao, kwa kule kutojimimina kwa uongozi ulio juu yao. Ieleweke wazi kuwa, Mungu ameuweka uongozi katika kanisa, ili kuwakamilisha au kuwabariki waamini katika kanisa la mahali. Kama waamini watakuwa wanawapenda viongozi wao na kutiririka pamoja nao, Mungu atawatumia viongozi hao kuwa majibu ya maswali yanayoyasonga maisha yao.


Heshima ya wana wa manabii kwa kiongozi wao

“Kisha wana wa manabii wakamwambia Elisha, angalia basi mahali tukaapo mbele yako ni padogo kwetu. Basi twende mpaka Yordan, twakuomba, tutwae huko kila mtu mti mmoja, ili tujifanyie huko mahali pa kukaa.” 2 Wafalme 6:1-2

Jambo la pili, tunalojifunza katika andiko hili, ni heshima waliyokuwa nayo hawa wana wa manabii kwa kiongozi wao. Andiko letu hapo juu linaonyesha kuwa, ingawa jambo walilotaka kulifanya halikuwa na kasoro yoyote, bado walitaka lipate kibali cha kiongozi wao. Hali hii ni tofauti kabisa na ilivyo kwa waamini wengi wa kanisa la siku hizi za mwisho.  Katika siku hizi za ukingoni mwa siku za mwisho, mwamini anaweza kufanya maamuzi makubwa katika maisha yake, bila hata kuona umuhimu wa kumshirikisha kiongozi wa kanisa lake la mahali. Mwamini wa jinsi hii anaweza kutoweka katika ibada kwa kipindi fulani, na siku utakapoamua kufuatilia aliko, utasikia kuwa, amehamia ushirika mwingine.

Maamuzi kama haya na mengine yanayofanana na hili,  yanaonyesha vile waamini wa jinsi hii, wasivyouheshimu uongozi katika kanisa lao la mahali. Kinachosikitisha katika hili ni kuwa, baadhi ya waamini hawawezi na hata wengine wamelala kabla ya wakati wao, kutokana na kutowaheshimu viongozi wa makanisa yao ya mahali. Tukumbuke kuwa, kiongozi yeyote yule aliyewekwa na Mungu ni mzazi, na katika hili maandiko yanasema, “waheshimu wazazi wako ili siku zako za kuishi, zipate kuwa nyingi, katika nchi akupayo BWANA Mungu.” Kama unataka baraka tele kutoka kwa Mungu, waheshimu viongozi wa ngazi zote wa kanisa lako la mahali.


Kiu ya kutaka kuandamana na uwepo wa Mungu

…Uwe radhi, basi nakusihi, uende pamoja na watumishi wako.” 2 Wafalme 6:3

Kitu kingine tunachojifunza katika andiko hili ni kuwa, wakati muujiza huu ulipotokea, kiongozi wa manabii ndiye aliyekuwa mwakilishi wa Mungu katika Israeli. Mara kwa mara watu walipohitaji kitu au kujua jambo fulani kutoka kwa Mungu, walienda kuuliza kwa mtu wa Mungu(nabii). Kutokana na nafasi ya nabii katika taifa hili teule la Mungu, tunaweza kusema kuwa, mahali popote alipokwenda nabii, hapo pia ulienda uwepo wa Mungu. Kutokana na ukweli huu, ombi la wana wa manabii la kuandamana na kiongozi wao, ndani yake lilibeba kutaka kuandamana na uwepo wa Mungu. Katika hili, tunaweza kusema kuwa, kwa yeyote anayetaka kukiona chuma kikielea katika maisha yake, ni lazima ahakikishe kuwa, anaambatana na uwepo wa Mungu kila mahali na wakati wote. Hili ni muhimu, kutokana na ukweli kuwa, katikati ya uhitaji, ndipo Shetani anapofanya kila mbinu, ili kumtoa mhitaji katika uwepo wa Mungu.

Ni vema tutambue kuwa, katika miaka tuliyo nayo, Elisha wetu ni neno la Mungu pamoja na Roho Mtakatifu. Kutokana na ukweli huu, tunapotii neno la Mungu na kutii kile Roho Mtakatifu anachotuagiza na kutufunza, tutakuwa tunaupa nafasi uwepo wa Mungu kuandamana nasi, tayari kukifanya chuma kielee katika maisha yetu.


KUWE NA KILIO KINACHOHITAJI MSAADA

“Ole wangu! Bwana wangu, kwani kiliazimwa kile.” 2 Wafalme 6:5

Jambo lingine lililochangia kuanzisha safari ya muujiza wa chuma kuelea, linapatikana katika kilio kilichotolewa na mhusika katika muujiza huu. Baada ya chuma cha shoka kuponyoka na kuzama mtoni, alitoa kilio mithili ya yule kipofu Bar Timayo. Kilio hiki kinatufundisha mambo makubwa mawili:-

Uaminifu wa mhitaji

Kitu cha kwanza tunachojifunza kuhusiana na kilio hiki, ni uaminifu aliokuwa nao huyu mwanafunzi katika chuo cha manabii. Shoka halikuwa lake na alikuwa anafikiria mara mbilimbili, jinsi atakavyokabiliana na mwenye shoka akiwa mikono mitupu. Ukweli huu unayahusu pia maisha yetu kama wanadamu na watoto wa Mungu. Neno la Mungu linasema wazi kuwa, “nchi na vyote viijazavyo, ni mali ya Mungu.” Zaburi 24:1. Kwa kusema hivi,neno la Mungu linatuonyesha kuwa, hata mwanadamu na vyote alivyo navyo, ni mali ya Mungu. Hali kadhalika neno la Mungu linatuambia wazi kuwa, “Sisi ni mali ya Mungu.” 1 Wakorintho 6:19.

Kwa vile sisi na vyote tulivyo navyo si mali yetu kulingana na maandiko, pale mambo yanapotatizika katika maisha yetu, ni lazima kusikitika kuonekane ndani yetu. Kusikitika huku, kunaonyesha kuwa, tunajali mali ya Mungu ambayo sisi tu mawakili wa mali hiyo. Sisi ni mali ya Mungu na tusingependa kuiona mali ya Mungu ikikaa katika hali ya kuharibika.

Mipaka ya uwezo wa kibinadamu

Jambo la pili, lililbebwa na kilio cha mwanafunzi huyu katika chuo cha manabii, ni ile mipaka ya uwezo wake kama mwanadamu. Sambamba na kilio chake kuonyesha kutokuwa na uwezo wa kufidia hasara iliyotokea, kinaonyesha pia kufikia mwisho kwa milango yake ya ufahamu. Kama angelikuwa na la kufanya, ni wazi asingekipeleka kilio chake kwa ‘mtu wa Mungu.’ Kwa maneno mengine, kibinadamu alikuwa hana uwezo wa kukipata chuma hicho.

Kama tunahitaji kuona chuma kikielea katika maisha yetu, ni lazima tuelewe nafasi ya milango ya ufahamu katika maisha yetu pamoja na mipaka yake. Watu wengi hawaoni vyuma vikielea katika maisha yao kutokana na kutojitutumua katika mambo yanayohitaji milango mitano ya ufahamu, na pia, kutokana na kujitutumua katika mambo yasiyohitaji milango hiyo ya ufahamu. Katika maisha haya chini ya jua, yako mambo yanayohitaji bidii za kimwili na yako mengine yanayohitaji kumwangalia Mungu peke yake. Kutokana na ukweli huu, kanisa linatakiwa kutambua mipaka yake kuhusiana na hitaji alilo nalo. Kama ni hitaji linaloweza kumalizwa na juhudi za kibinadamu, basi juhudi hizo ziwekwe na kama haliwezekani kibinadamu, mwamini akielekeze kilio chake kwa Mungu. Hivi ndivyo yule mwana wa nabii alivyofanya, alitambua mipaka ya ubinadamu wake, pale shoka lilipomponyoka. Mara zote uwezo wa milango ya ufahamu inapofikia mwisho katika kutenda, ndipo Mungu anapoingilia na kukutana na mahitaji ya mtu.


KUYAFAHAMU MAZINGIRA YA HITAJI

“Mtu wa Mungu akasema, kilianguka wapi? Akamwonyesha mahali.” 2 Wafalme 6:6

Kuelewa mahali chuma kilipoangukia kulikuwa ni kwa muhimu mno kuhusiana na muujiza mzima wa kuelea kwa chuma cha shoka. Watu wengi wanashindwa kuona vyuma vikielea katika maisha yao kutokana na kutokuwa na ujuzi wa kutosha kuhusu mahitaji yao. Mfano mzuri katika hili, tunaweza kuuona kwa kumwangalia mgonjwa aliyeamua kwenda katika hospitali inayohudumiwa na madaktari wanaofuata miiko ya uganga.  Mgonjwa anapofika katika mojawapo ya hospitali hizi, matibabu ya kwanza anayopewa, ni kupewa nafasi ya kutosha kueleza kile kinachomsumbua. Hapo ndipo mgonjwa atakapopata nafasi kwa upana kuelezea kile kinachomsumbua na aina ya matibabu aliyokwisha kuyapitia. Baada ya kukamilisha maelezo yake, bado daktari hataanza kumpatia matibabu mpaka pale atakapomfanyia mgonjwa huyo uchunguzi wa kina, kuhusiana na ugonjwa unaomkabili mgonjwa. Hivi ndivyo inavyotakiwa kufanyika pale tunapolipeleka hitaji letu kwa Mungu. Tunatakiwa kumwendea tukiwa na mzizi wa tatizo badala ya matawi ya tatizo.

Wakati mwingine ili kupata ufahamu wa kutosha juu ya kile tunachohitaji, ni vema tuhakikishe kuwa tunakuwa na neno linaloendana na kile tunachohitaji ili tumwambie Mungu kuwa, tunahitaji kukiona chuma kikielea kulingana na andiko hili. Katika hili tuelewe kuwa, neno la Mungu linasema wazi kuwa, “Mungu huliangalia neno lake apate kulitimiza.” Yeremia 1:12. Wakati mwingine kukokosa ujuzi wa kutosha kuhusiana na tatizo lake, ndiko kunakowafanya waamini wengi kuwa na mzunguko mrefu wakati wa kupeleka mahitaji yao mbele za Mungu.

Elisha alimtaka yule mwana wa nabii kuonyesha pale chuma kilipodondokea na aliyatumia maelezo hayo, kutumbukiza kijiti mahali pale pale chuma kilipoangukia.


MAPENZI YA MUNGU KUHUSIANA NA HITAJI

“Ole wangu! Bwana wangu, kwani kiliazimwa kile.” 2 Wafalme 6:5

Jambo lingine lililobebwa na kilio hiki cha mwana wa nabii, ni wema aliokuwa nao kuhusiana na shoka lile aliloliazima. Wema huu ni ile hali ya kutambua kuwa, ilikuwa mapenzi ya Mungu kumrudishia mwenyewe shoka alilokuwa ameliazima kwake. Katika hili wako waamini walio wepesi kuazima au kukopa kwa watu ila unapofikia wakati wa kurejesha, inakuwa ‘mshike mshike na nguo kuchanika!’ Kama kitu kimeazimwa kwa mtu, ni mapenzi ya Mungu kirudishwe kwake kikiwa katika hali nzuri. Hali ya mhitaji kuyaelewa mapenzi ya Mungu kuhusiana na kile anachokihitaji, kutainua kiwango cha imani katika kuomba na kupokea. Kutokana na ukweli huu, kabla ya kutaka kuona chuma kikielea, ni vema kwanza mhitaji ayaelewe mapenzi ya Mungu kuhusiana na hitaji lake. Wakati mwingine ili kuwa katika mapenzi ya Mungu wakati wa kuomba, mhitaji anatakiwa aombe ushauri kwa kiongozi wake wa kiroho.


KUELEA KWA CHUMA KUNAHITAJI IMANI

“Mtu wa Mungu akasema, Kilianguka wapi? Akamwonyesha mahali. Akakata kijiti, akakitupa pale pale, chuma kikaelea.” 2 Wafalme 6:6

Baada ya Elisha kuelezwa juu ya kudondoka kwa chuma mtoni, alitaka ufafanuzi kuhusiana na mahali kilipodondokea. Badala ya Elisha kulia pamoja na mwana wa nabii, yeye alitaka ufafanuzi wa pale chuma kilipodondokea. Mara zote mtu hudodosa undani wa jambo, pale anapokuwa na imani ya kufanyika kitu fulani kuhusiana na tatizo hilo. Baada ya yule mwana wa nabii kuulizwa na Elisha pale chuma kilipoangukia, alionyesha sehemu kilipoangukia kuonyesha kuongezeka kwa kiwango cha imani yake. Hii ndiyo kazi ya viongozi katika huduma yoyote ile, wamewekwa na Mungu ili kuwainua watu, pale wanapozimia kiimani. Kwa imani ya Elisha alichukua kijiti (point of contact) na kukitupa mahali chuma kilipoangukia na chuma kikaelea.

Mpendwa, huu ndio mfululizo wa mambo yaliyosababisha kuelea kwa chuma wakati wa Elisha. Kwa Mungu ni yeye yule jana, leo na hata milele, kama kuna sehemu ya maisha yako iliyozama majini, anao uwezo wa kuifanya ielee tena. Unachotakiwa kufanya ni kuyatendea kazi kwa imani, yale yote uliyojifunza katika somo hili. Ukiwa na swali lolote, unaweza pia kuwasiliana nasi na tutakusaidia pamoja na kuomba pamoja nawe. AMENI!